Friday, January 28, 2022

Waziri Mkenda avutiwa na DIT Kuwa na Kampuni Tanzu Kwa ajili ya kubiasharisha teknolojia





Na Mathias Canal, Dar es salaam

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia,  Prof. Adolf Mkenda ameipongeza Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa kuwa na Kampuni Tanzu ya Taasisi ambayo kazi yake ni kubiasharisha teknolojia na bunifu zinazobuniwa na wataalamu wa Taasisi hiyo.


Aidha, Waziri huyo ameagiza DIT kupitia Kampuni hiyo kuanza kutengeneza vipuri vya vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na magari, bajaji na pikipiki ili kusaidia bidhaa hizo kuanza kupatikana hapa nchini badala ya kuagizwa kutoka nje.

"Niipongeze sana DIT kwa kweli wamefanya kitu kikubwa sana kuanzisha Kampuni yao ambayo inawasaidia kupeleka hizi bunifu sokoni, hiki ni kitu kikubwa sana, lakini niwashauri muanze kutengeneza vipuri hivi vya bajaji, pikipiki ambavyo vinauzika haraka," amesema Prof. Mkenda.

Waziri Prof. Mkenda amesema hayo leo alipotembelea DIT ikiwa ni ziara yake ya kwanza kwa Taasisi hiyo ya kukagua na kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na DIT. Katika ziara hiyo ameambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. James Mdoe, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi,  Dkt. Noel Mbonde na Mkurugenzi wa Idarq ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu,  Prof. Maulilio Kipanyula.

Prof. Mkenda amesema kuanza utengenezaji wa vitu hivyo unaweza kuwa mgumu lakini Wizara yake inaahidi kuendelea kusaidia kutatua changamoto zitakazokuwepo ili jambo hilo lifanikiwe.

"Tunahitaji bidhaa kama hivi vipuni na niwaambie mwanzoni inaweza kuwa ngumu na isiwe na faida kubwa lakini niwahakikishie kwamba kama Wizara tutawasaidia kuhakikisha hili linafanikiwa kwasababu tunapoteza pesa nyingi kuagiza vipuri kutoka nje ya nchi," amesema.

Prof. Mkenda amesema kuwa Taasisi za ufundi ni muhimu katika uchumi wa nchi kwani zinazalisha ajira na kuongeza teknolojia na hivyo kuondoa utegemezi wa kununua vitu kutoka nje.

Aidha, Prof. Mkenda amepongeza pia DIT kwa kubuni na kutengeneza vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na mashine mbalimbali, kiti cha kumsaidia kukaa na kusimama mlemavu wa miguu pamoja na mifumo mbalimbali.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Tanzu ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT Co Ltd), Joseph Challo akielezea kampuni hiyo, amesema kazi ya kampuni ni kuboasharisha bunifu mbalimbali zinazobuniwa katika Taasisi hiyo ambapo mpaka sasa kampuni inajivunia kuingiza sokoni ubunifu wa taa za kuongozea magari na watembea kwa miguu pamoja na bunifu za mashine mbalimbali.

Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Prof Preksedis Ndomba amemuahidi Prof Mkenda kuwa maelekezo yote aliyoyatoa yamepokelewa na yatatekelezwa kwa maendeleo ya Taasisi pamoja na taifa kwa ujumla. 



Mwisho

 

No comments:

Post a Comment