Friday, January 14, 2022

WAZIRI MHAGAMA AKABIDHI RASMI OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MAWAZIRI WAPYA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi Nyaraka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Joyce Ndalichako kama ishara ya kumkabidhi rasmi ofisi hiyo, kulia ni Waziri wa Nchi anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge Mhe. Dkt. Pindi Chana tarehe 13 Januari, 2022 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama akimkabidhi Nyaraka Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Mhe. Dkt. Pindi Chana kama ishara ya kumkabidhi rasmi ofisi hiyo, kulia tarehe 13 Januari, 2022 katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Joyce Ndalichako na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama wakiweka saini nyaraka za ofisi hiyo kabla ya makabidhiano rasmi ya ofisi hiyo.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) Mhe. Dkt. Pindi Chana wakiweka saini nyaraka za makabidhiano ya ofisi hiyo wakati wa hafla hiyo.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama  amekabidhi rasmi ofisi kwa Waziri  wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Dkt. Pindi Chana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako  ili kuendelea na majukumu katika ofisi hiyo.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano  ya ofisi hiyo Januari 13, 2022 Jijini Dodoma Mhe. Mhagama alimshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa kuhudumu nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka saba  ambapo  amewashukuru watumishi kwa ushirikiano walioutoa wakati wote wa utekelezaji wa majukumu kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa watumishi kupitia  nafasi aliyoteuliwa kutumikia  ya Ofisi ya Rais  Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Ubora kwa kuendelea kutatua changamoto za watumishi wa umma , kusimamia haki za watumishi wa umma kuhakikisha wanatumikia wananchi kwa weledi kwa ustawi wa Taifa.

“Ninajua kiu ya watumishi wa umma ndani ya Nchi yetu, ninajua vilio vya madaraja ninajua vilio vya watendaji ambao wakati mwingine hawataki kutoa haki kwa watumishi wa umma ninajua masuala yote yaliyowekwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi wa umma ninaomba niwaambie bado ni sehemu ya utendaji wa kazi wa Serikali ili yale mambo yanayohusiana na utumishi wa umma nipo bado pamoja na nyie,” alisema Mhe. Mhagama.

Hata hivyo aliwasihi watumishi hao kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mawaziri walioteuliwa katika Ofisi hiyo pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na weledi kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla na wananchi wake.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Bunge Mhe.  Dkt. Pindi Chana alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumteua kutumikia nafasi hiyo huku akiahidi kufanya kazi kwa bidii na utayari wake kushirikiana na watumishi wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yake.

Katika hatua nyingine Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu  Mhe. Prof. Joyce Ndaliachako aliwaomba watumishi wa ofisi hiyo kufanya kazi kwa mshikamano kuhakikisha Taifa linapata maendeleo na wananchi wake na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Kwa upande wake aliyekuwa Katibu Mkuu  Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu  Tixon Nzunda amekabidhi ofisi kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Dkt. John Jingu  na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu.

Akiaga watumishi wa ofisi hiyo Katibu Mkuu Nzunda aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu  Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia sekta ya Mifugo alimshukuru Mhe. Rais wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu kwa kumuamini na kumruhusu kuendelea kuwatumikia wananchi .

“Nataka niwahakikishie  Makatibu Wakuu wenzangu timu hii mnayoiona ni nzuri na itawapa ushirikiano , timu imara, ni watu wanaofanya kazi usiku na mchana kwa hiyo nawapongeza kwa kuungana na familia ya ofisi ya Waziri Mkuu kwahiyo ninaomba ushirikiano mliokuwa mnanipa mkawape makatibu hawa kuhakikisha ile misingi ya uwajibikaji na weledi inaendelezwa,” alisema Nzunda.

Sambamba na hilo Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Bunge Dkt. John Jingu alieleza kwamba fursa hiyo kwake ni nafasi muhimu ya kutoa mchango wa maendeleo ya Taifa huku akiwasisitiza watumishi hao  kuwa huru kutoa maoni yao kwa lengo la kuboresha, kujenga na kuimarisha shughuli za uratibu wa Serikali.

“Namshukuru Mhe. Rais kwa kuona naweza kutoa mchango kwa kuhudumu Pamoja nanyi katika ofisi hii niwaombe ushirikiano maana kila mmoja hapa ni gwiji katika eneo lake na nimekuja kufanya kazi na nyie. Moja ya kazi yangu ni kujifunza kutoka kwenu ili twende pamoja mlango uko wazi ukiwa na wazo unalofikiri litachangia katika kuboresha utendaji wetu wa kazi nakukaribisha kutoa maoni yako ili twende na kasi ya Awamu ya Sita,”alibainisha Dkt. Jingu .

Vile vile Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamal Katundu aliahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa watumishi kuhakikisha ndoto ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwafikia wananchi kwa huduma bora inafikiwa.

Aidha Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Uratibu na Bunge Bw. Kasper Mmuya alieleza furaha yake ya kuendelea kuhudumu katika ofisi hiyo huku akiwaasa wafanyakazi kutumia muda wao vizuri wawapo kazini kwa kuhudumia na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi wakizingatia taaluma walizonazo.

No comments:

Post a Comment