Monday, January 24, 2022

WAZIRI JAFO AHAMASISHA UHIFADHI WA MISITU KULINDA MAZINGIRA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo akiwa katika ziara ya kutembelea na kukagua shughuli za uhifadhi wa msitu wa Tongwe uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi ambao unahifadhi wa kupitia mradi wa hewa ya ukaa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo akiwahimiza wanafunzi wa Shule ya Msingi Vikonge kupanda mti mmoja kwa kila mwanafunzi na kuutunza alipofanya katika ziara wilayani Tanganyika mkoani Katavi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo akishiriki zoezi la kupanda mti na wanafunzi wa Shule ya Msingi Vikonge wilayani Tanganyika mkoani Katavi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo akiangalia msitu wa Tongwe uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi uliovyohifadhiwa na kutoa faida za kimazingira alipofanya ziara ya kikazi.

Sehemu ya msitu wa Tongwe uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi uliovyohifadhiwa na kutoa faida za kimazingira alipofanya ziara ya kikazi.

Na Robert Hokororo, Katavi

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi kwa kulinda msitu wa Tongwe unaosaidia katika kuzalisha hewa ya ukaa na hivyo kuhifadhi mazingira.

Ametoa pongezi hizo Januari 23, 2022 alipofanya ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua msitu huo wa kijiji ulioingizwa katika Mradi wa Hewa ya Ukaa kupitia Taasisi ya Carbon Tanzania.

Dkt. Jafo alisema kuwa msitu huo unapaswa kuwa sehemu ya mfano ya kujifunzia kwa halmashauri zingine kwa kuwa unaunga mkono jitihada za nchi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Hapa nawasifu, naona kuna maporomoko ya maji nah ii ni kutokana na namna mnavyoutunza msitu huu maana leo hii kule Morogoro katika milima ya Uluguru hakuna maji yanayotiririka na ndio maana Bwawa la Mindu limekauka na wameingia katika mgao wa maji yote haya ni kutokana na uharibifu wa mazingira,” alisema.

Aidha, Dkt. Jafo alimuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko kukaa na Halmashauri hiyo pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) namna bora ya kuusimamia kwa pamoja ili dhana ya uhifadhi wa mazingira ifanikiwe.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu katika taarifa yake alisema mradi huo umelenga kuhifadhi mazingira, bioanuai zote muhimu na zilizo hatarini kutoweka pamoja vyanzo vya maji na wanyapori.

Buswelu alisema kuwa pia mradi unalenga kuboresha huduma kwa jamii pamoja na kuihusisha katika uhifadhi na kunufaika moja kwa moja na faida zitokanazo na shughuli za uhifadhi.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya alibainisha changamoto zikiwemo uvamizi wa maeneo ya misitu na kuendelea kufanya uharibifu kwa kukata miti hatua inayoweza kusababisha changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Pia aliongeza kuwa baadhi ya viongozi wa vijiji kushirikiana na wahalifu wanaofanya shughuli zisizo rafiki uhifadhi wa misitu pamoja na maeneo ya malisho yaliyotengwa na wanancgi wenyewe.   

Hewa ya ukaa inapatikana katika misitu ya asili iliyohifadhiwa vizuri ambayo inaweza kunyonya na kuhifadhi hewa ya ukaa na hivyo aliyehifadhi misitu hiyo hupata ruzuku kutoka mataifa yanayozalisha kabonidayoksaidi.

Katika hatua nyingine Waziri Jafo akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Vikonge alisisitiza kila mwanafunzi kupanda mti mmoja na kuutunza ili kutimiza lengo la kupanda miti takriban milioni 14.

No comments:

Post a Comment