Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa ubia baina ya Serikali na kampuni ya Barrick (Barrick Gold Corporation) uliounda kampuni tanzu ya Twiga (Twiga Minerals Corporation Limited) umeleta tija kubwa katika sekta ya madini nchini.
Waziri Dkt. Biteko ameyasema hayo Januari 25, 2022 alipotembelea mgodi wa Bulyanhulu uliopo Halmashauri ya Msalala Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ikiwa ni miongoni mwa migodi inayoendeshwa na kampuni ya Twiga kwa ubia baina ya Serikali yenye asilimia 16 na Barrick yenye asilimia 84.
Amesema ubia huo umechochea fursa zaidi za ajira kwa watanzania ambapo katika mgodi wa Bulyanhulu zaidi ya asilimia 96 ya wafanyakazi ni watanzania ambapo asilimia 41 wanatoka katika maeneo yanayozunguka mgodi.
Aidha Waziri Dkt. Biteko ameongeza kuwa hatua hiyo imechochea ongezeko la makusanyo ya Serikali katika Sekta ya madini kutoka chini ya shilingi 115 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 528 mwaka 2020/21 huku pia ikifungua ubia zaidi baina ya Serikali na makampuni mengine.
Katika hatua nyingine Dkt. Biteko amewatoa hofu wafanyakazi katika mgodi wa Bulyanhulu kuwa hawatapoteza ajira zao kufuatia mabadiliko yanayofanywa na mgodi huo kutoka kwenye mitambo inayoendeshwa na binadamu chini ya mgodi kwenda kwenye mitambo inayoendeshwa kwa kompyuta (automine) kwani bado watakuwa na fursa ya kuendesha mitambo hiyo wakiwa ofisini.
Kwa upande wake Rais na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Barrick duniani, Dkt. Mark Bristow amekiri kuwa ubia baina ya Serikali ya Tanzania na kampuni yake umeleta tija kubwa hususani uzalishaji katika migodi ya Bulyanhulu na North Mara hadi kufikia wakia laki tano za dhahabu hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana 2021 huku ukiifanya migodi hiyo kuwa na hadhi ya kimataifa.
Naye Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Dkt. Sophia Mjema amesema atahakikisha mgodi unashirikiana kwa ukaribu na Serikali za Mitaa/ Halmashauri na kwa kuwashirikisha wananchi ili kuibua miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) itakayokuwa na tija badala ya kusubiri kuletewa miradi bila makubaliano ya pamoja.
Ziara ya Waziri Dkt. Biteko katika Halmashauri ya Msalala ilitamatika katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kakola ambapo alitumia fursa hiyo kusisitiza kuwa Serikali imeweka msisitizo wa kuhakikisha wananchi wananufaika na uwepo wa mgodi wa Bulyanhulu huku ikihakikisha wenye madai halali ya fidia ikihakikisha wanalipwa.
Waziri wa Mdini, Dkt. Doto Biteko akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Kakola Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama.
Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Dkt. Sophia Mjema.
Rais na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Barrick duniani, Dkt. Mark Bristow akiwa kwenye kikao baina yake na Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko (hayuko pichani).
Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye kikao hicho.
Wafanyakazi wa mgodi wa Bulyanhulu wakiendesha mitambo ya kuchoronga miamba ya madini chini ya mgodi kwa kutumia mfumo wa kidigitali (automine) wakiwa ofisini.
Waziri wa Madini, Dkt. Dkt. Biteko pamoja na ujumbe alioambatana nao akiangalia mfumo wa kidigitali uliofungwa katika mgodi wa Bulyanhulu kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kuchoronga miamba ya madini chini ya mgodi kwa kutumia kompyuta (automine).
No comments:
Post a Comment