Wednesday, December 15, 2021

WALIOSAFIRISHA MADAWA YA KULEVYA RUMBESA 48 WANASWA SINGIDA , ACP MUTABIHIRWA ATOA TAMKO









Na Hamis Hussein - Singida 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limefanya msako kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama  na kufanikiwa  kuwakamata wahalifu wanaojihusisha na biashara ya madawa ya kulevya na wizi wa vitu mbalimbali ikiwemo pikipiki Tv na sabufa kuanzia mwezi  Novemba tarehe 18 hadi jana  Desemba 14,mwaka huu.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ya kuwakamata wahalifu hao Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Mutahibirwa amesema kuwakamata mahalifu hao ni mafanikio makubwa kwa jeshi hilo.

Kuhusu madawa ya kulevya ACP Mutahibirwa amesema kwa kipindi hicho wamefanikiwa kukamata madawa aina ya bhangi misokoto 667 na mbegu za bhangi kg. 1 ambapo walikamatwa  watuhumiwa watatu, akiwemo mtuhumiwa wa kiume anayetambulika kwa jina la Manjoli Manjoli (52) Mkazi wa Mtaa wa Utemini Singida ambaye alikamatwa akiwa na misokoto 550 ya bhangi na kuwa watuhumiwa hao ni wauzaji na watumiaji wa bhangi.

Amesema jeshi hilo la polisi lilikamata watuhumiwa wakiwa wanasafiri na madawa ya kulevya wakitokea mwanza kuelekea mkoani singida wakiwa wamebeba rumbesa ya madawa kwa kificho cha hali ya juu.

“Kutokana na taarifa za kiintelijensia ambazo tumeweza kuzipata  tulifanikiwa kuwapata wakiwa na mabegi mawili ambao walikuwa wameweka rumbesa hizo 48 na juu yake wakaweka nguo ili kupoteza lengo au kumfanya mtu asitambue nini amebeba , kama mnavyofahamu mkoa wetu wa singida tumezungukwa na barabara nyingi kubwa za wasafiri wengi wanapita kwenda mikoa mbalimbali,kwahiyo hawa wanawake wawili walikuwa wanasafirisha rumbesa 48 kupeleka  kwenye migodi ilipo mkoa wetu wa singida ”  Alisema ASC Mutabihirwa.

Sanjali na msako huo uliokamata watuhumiwa waliokuwa wakisafirisha madawa ya kulevya kutoka mwanza kuelekea singida pia msako huo umewakata watumiwa wanne wa wizi wa pikipiki ambao kesi zao zilishafikishwa mahakamani.

Vilevile katika misako kwa kipindi hicho tuliweza kuwakamata watuhumiwa wanne ambao ni wezi wa pikipiki , watuhumiwa hao tayari  wameshafikishwa mahakamani  na mmoja kati yao ameshahukumiwa  kwenda jela na kesi zilizobakia zipo katika hatua ya mwisho , vilevile tuliweza kukamata TV 2  subufa 2 ambacho katika hizo tutaomba wananchi wa mkoa wa singida  kujitokeza ili  kutambua mali zao kama zitakuwa ni za kwao.”. Aliongeza kamanda Mutabihirwa

Kadhalika ACP Mutabihirwa alitumia nafasi hiyo kuwashukuru raia wema na kuwa mafanikio hayo yametokana na taarifa za kiintelijensia zilizotolewa na raia wema wanaopenda Mkoa wa Singida na kutoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa huo  kuachana na biashara haramu na badala yake wafanye kazi halali vilevile kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu .

"Wananchi wanatakiwa kuachana kabisa na biashara haramu zikiwemo biashara za dawa za kulevya aina mbalimbali badala yake wafanye kazi halali ambazo ziotawapatia kipato" aliongeza  ACP Mutahibirwa.

 

 

No comments:

Post a Comment