Friday, December 3, 2021

DKT. GWAJIMA APOKEA DOZI 115,200 ZA JANSSEN








Na WAMJW-DSM 

Tanzania imepokea shehena ya Chanjo aina ya Janssen Dozi 115,200 zitakazotumika kuchanja wananchi 115,200 kwa ufadhili wa Serikali ya Ubeligiji kupitia mpango wa COVAX Facility kwa lengo la kuwakinga wananchi dhidi ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa virusi vya UVIKO-19. 

Akizingumza na waandishi wa habari katika uwanja wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es salaam baada ya kupokea Chanjo kutoka kwa Balozi wa Ubeligiji nchini Tanzania Peter Van Acker Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa, Serikali itaendelea kutoa chanjo dhidi ya UVIKO-19 katika vituo mbalimbali vya Afya hapa nchini kwa mujibu wa miongozo iliyopo ili kuwezesha wananchi kujikinga dhidi ya UVIKO-19. 

Amesema kuwa, awamu ya kwanza Serikali ilipokea dozi 1,058,400, awamu ya pili dozi 169,000 na leo Desemba 3, 2021 hivyo kufanya jumla ya Chanjo aina ya Janssen zilizopokelewa hapa nchini kufikia Dozi 1,342,600 na kufanya jumla ya chanjo zote zilizopokelewa kuwa  dozi 4,421,540 zikiwemo chanjo ya Sinopharm na Pfizer ambazo zitachanja watu 2,882,545 . 

Aidha Dkt Gwajima amewaagiza viongozi na watendaji wa ngazi zote kutoa ushirikiano wa hali ya juu kuhamasisha jamii kujitokeza kupata chanjo na  kisha kujikinga kwa kuchukua tahadhari dhidi ya Uviko 19 ikiwa ni pamoja na uvaaji wa barakoa, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono (Sanitizer), kufanya mazoezi na kuepuka misongamano isiyo yalazima. 

No comments:

Post a Comment