Wilaya ya Kwimba Mkoani
Mwanza katika msimu mpya wa kilimo cha zao la pamba mwaka 2021/2022 imejiwekea
mikakati mbalimbali ili kuhakikisha inafikia malengo waliyowekewa na serikali
ya kuzalisha tani 30,000.
Katika kufikia malengo
hayo Wilaya hiyo kwa kushirikiana na balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey
Mwanri wamekuwa wakifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa wananchi
kuhusu kilimo bora cha zao hilo kwa kutumia vipimo vipya ambavyo vimefanyiwa
utafiti na kituo cha utafiti cha Ukiriguru.
Akizungumza na City fm
Radio na City Digital iliyotaka kufahamu
mikakati gani ambayo wilaya imekuja nayo, Mkuu wa wilaya ya Kwimba Johari Mussa
Samizi alisema mbali na elimu kutolewa
na balozi watahakikisha maafisa ugani kwa kushirikiana na maafisa wa kilimo na
umwagiliaji wa wilaya wanazungukia wakulima wote katika hatua zote za awali
kuhakikisha wanatumia maarifa yote waliyopata.
“Kihistoria Wilaya ya
Kwimba ndo ilikuwa kinara wa uzalishaji wa zao la pamba hapa nchini, sasa
tumepitia changamoto nyingi ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi lakini sasa
tumeamua kuhakikisha kwamba Kwimba inarudi kwenye nafasi yake na hili linawezekana”.
Alisema
“Kama unavyofahamu
upandaji unatarajia kuanza Novemba 15 kwahiyo kwa sasa tupo katika kuhakikisha
wananchi wote wanafatilia mafunzo haya ikiwemo vipimo vipya vya upandaji
ambavyo ni sentiminta 60 kwa 30 na kwa mujibu wa wataalamu kupitia vipimo hivi
tutaongeza uzalishaji tofauti na vile ambavyo vilitumika awali”. Aliongeza
“ Mbali na vipimo kwa
kushirikiana na balozi wa zao la Pamba wakulima wameelekezwa namna bora ya
kuanda mashamba na uzuri elimu hii ilianza kutolewa na wataalamu wa kilimo
kutoka wilayani na mpaka kufikia hatua hii sasa ya upandaji na tunaamini kwa
kuzingatia hili mwakani wilaya yetu itafanya maajabu makubwa sana.”
Kwa upande wake afisa
kilimo na umwagiliaji wilayani humo Mhandisi Magreth Kavalo amelitaja zao la
Pamba kuwa ni moja wapo ya mazao ya biashara wilayani humo, na kuwataka
wakulima kuzingatia mafunzo yote yaliyotolewa na balozi wa Pamba kwa ajili ya
kuongeza tija katika zao hilo.
“Lengo kuu tulilonalo
kwa sasa ni kuongeza tija kwenye uzalishaji kutoka kilo 100, 200 na 300 na
katika hilo tumeanza mikutano ya uhamasishaji kupitia maafisa ugani, maafisa
kilimo na maafisa kutoka halmashauri pia
tumeunda vikundi vya wakulima
wahamasishaji tunawafundisha mbinu za kilimo bora na hasa zile kanuni kumi bora
za kilimo cha zao la pamba ili wawafikie
wakulima kwenye maeneo mbalimbali.”
Aidha amewata wakulima
wilayani humo kuwasiliana na idara ya kilimo nha umwagiliaji kila wanapokutana
na changamoto yoyote katika hatua za kilimo cha zao hilo nao wako tayari katika
kumshika mkulima mpaka kufikia lengo walilojiwekea.
Katika kuhakikisha
wakulima wa wilaya ya Kwimba wanafikia malengo yao, Bodi ya Pamba Tanzania
imegawa pikipiki kwa maafisa ugani, imesambaza mbegu za kutosha , imegawa
mifuko ya kubebea, imetoa kamba za vipimo
pamoja na kutoa elimukwa wakulima kupitia balozi wa Pamba nchini.
Naye Balozi wa zao hilo
nchini Aggrey Mwanri alisema baada ya utafiti wa zao hilo kutoka nchi
mbalimbali ikiwemo Senegal, Brazil, Benin , Sudan ambao wanazalisha heka moja
kilo 2500 lakini hapa kwetu mtu wa juu kabisa katika heka moja anatoa kilo 100
zimezidi sana 300.
Hivyo basi bodi ya
Pamba waliamua kufanya mabadiliko kwenye vipimo, lakini pia waligundua kuna
makosa mbalimbali yanayofanywa na wakulima na hivyo kuleta uzalishaji hafifu na
usio na tija.
“Tuligundua baadhi ya
wakulima hawaharibu masalio shambani,
hawapulizii vizuri dawa ya kuulia wadudu, hawapalilii vizuri, wengine
wanachanganya mazao Zaidi ya mawili katika shamba moja, wengine baada ya kulima
wanavuna vibaya na hivyo Pamba yetu inaonekana ni chafu dhidi ya mataifa
mengine yanayolima zao hilo.” Alisema
“Kupitia mafunzo haya
tumewaelekeza wakulima vipimo vipya, namna bora ya upuliziaji dawa za kuua
wadudu, namna bora ya kurudishia udongo kwenye mashimo, namna na ya kupalilia,
namna ya kuvuna na namna ya kutunza pamba pamoja na matumizi ya samadi.”
“Tunaamini kama wakulima watazingatia tutarajie uzalishaji mkubwa wa zao hili katika nchi yetu na tunaamini itakuwa hivyo kwani utafiti haudanganyi” alimalizia kusema.
No comments:
Post a Comment