Waziri wa Kilimo Mhe
Prof Adolf Mkenda na Bi. Amina Shaaban Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na
Mipango wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa majadiliano ya
kisera kwenye mazao ya mbegu za mafuta na faida za mradi wa uzalishaji umeme wa
maji ya Mwalimu Nyerere kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania, leo tarehe 4
Novemba 2021 Jijini Dar es salaam.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Serikali itaendelea kutekeleza mipango na mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya
mafuta. Kwa upande wa alizeti imeanza kutekeleza mpango wa kitaifa wa kuongeza
uzalishaji wa zao la alizeti kujitosheleza kwa mafuta ya kula nchini na kuokoa
fedha zinazotumika kuagiza mafuta ya kula.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda
ameyasema hayo tarehe 4 Novemba 2021 wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya
kisera kwenye mazao ya mbegu za mafuta na faida za mradi wa uzalishaji umeme wa
maji ya Mwalimu Nyerere kwa maendeleo ya uchumi wa Tanzania leo tarehe 4
Novemba 2021 Jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa Serikali imeweka mikakati
mbalimbali ya kuongeza uzalishaji na tija ya mazao ya mafuta.
Mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kuimarisha huduma za ugani kwa kuwapatia
vyombo ya usafiri maafisa ugani ikiwemo kununua pikipiki 1,500, vifaa maalum
vya kupimia udongo (Soil Test Kits),
visanduku vya ugani (Extention Kits),
simu janja na kuwezesha uanzishaji
wa mashamba ya mfano kwa kila afisa ugani na kutoa mafunzo rejea.
Amesema kuwa huduma
hizo zitawezeshwa kwa kuwa Wizara imeongeza bajeti ya Kuimairisha huduma za
ugani kutoka Shilingi milioni 603 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 11.5
mwaka 2021/2022. Katika utekelezaji wa mpango
huo, Wizara imechagua
Mikoa mitatu ya Kielelezo ambayo ni Singida, Dodoma na Simiyu yenye fursa kubwa
ya kuzalisha mazao ya mafuta hususan alizeti na pamba.
Waziri Mkenda amesema kuwa Katika mwaka 2021/2022
Serikali imeongeza bajeti ya Taasisi ya Utafiti Tanzania (TARI) kutoka Shilingi
bilioni 7.35 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni
11.63 mwaka 2021/2022. Vilevile, bajeti ya Wakala wa Mbegu wa Taifa (ASA)
kutoka bilioni 5.42 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi bilioni 10.58 mwaka 2021/2022
ili kuongeza upatikanaji wa mbegu bora zikiwemo mbegu za mazao ya mafuta.
Vilevile Amesema kuwa Wizara ya kilimo itaendelea kuhamasisha uanzishaji wa mashamba ya pamoja (block farming) katika mikoa inayozalisha mazao ya
mafuta kwa lengo la kurahisisha utoaji wa huduma ikiwemo mbegu bora, mbolea,
viuatilifu na zana bora za kilimo pamoja na mafunzo ya kilimo bora kwa
wakulima. Aidha, Serikali itaimarisha kilimo cha mkataba kwa mazao ya mafuta
kwa lengo la kuwa na uhakika wa masoko.
“Serikali itaendelea kuboresha
mazingira ya uwekezaji na kuondoa vikwazo vya kisera na kisheria ili kuhamasisha uwekezaji.
Maeneo ambayo tumeanza kuyafanyia kazi ni mfumo wa upatikanaji wa mitaji katika
sekta ya kilimo na masuala ya kikodi kwenye mazao ya
mafuta” Amekaririwa Waziri Mkenda
Amesema kuwa Tanzania ilikuwa ikitekeleza Mkakati wa Kuendeleza Zao la Alizeti kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi 2020. Malengo mahsusi yaliyoainishwa kwenye Mkakati huo ni pamoja na kuimarisha utafiti wa mbegu bora na kuboresha mazingira ya uwekezaji katika tasnia ya alizeti.
Ameyataja matokeo
yaliyopatikana kutokana na mkakati huo kuwa ni pamoja na Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo
Tanzania (TARI) imesafisha (purification) mbegu bora ya alizeti
aina ya Record ili kuongeza uzalishaji na tija; pamoja na kuidhinisha matumizi
ya mbegu bora 11 ambazo ni TARI-ILO2019, TARI-NA2019, Aguara4, Aguara6, Hysun33,
Supersun64, Supersun66, Michel, Ancilla, Archeo na Soleado.
MWISHO
No comments:
Post a Comment