Katika kuelekea Kilele
cha Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani, Waziri wa Madini Doto Biteko
ameitumia fursa hiyo kuwataka wachimbaji wote wa Madini Nchini kuhakikisha
wanalinda afya zao kwa kujikinga na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.
Waziri Biteko ameyasema
hayo baada ya kutembelea mgodi wa wachimbaji wadogo wa Nsungwa uliopo wilayani
Kaliua Mkoa wa Tabora ambako kumeibuka mfumuko wa Madini ya Dhahabu (Rush).
Aidha, Waziri Biteko
amewataka wachimbaji hao kuhakikisha wanatunza akiba ya kipato wanachokipata na
kutunza familia zao ikiwemo kuwekeza katika sekta nyingine hususan katika Sekta
ya Biashara na Kilimo.
“Hela unayoipata
usiidharau hata kama ni kidogo weka akiba ili ije ikusaidie kesho ukiwa huna
nguvu, leo unanguvu unaingia duarani lakini baada ya miaka kadhaa hautaweza,
utaitaji watu wa kukusaidia, nguvu ya leo uiweke akiba kwa ajili ya kesho ili
ikusaidi kuwa na kesho nzuri usije ukawasumbua watu,” amesema Waziri Biteko.
Waziri Biteko amesema
Wilaya ya Kaliua inafahamika kwa Kilimo cha Tumbaku ambapo kwa sasa umetokea
mlipuko wa Madini ya Dhahabu katika eneo hilo na kusababisha Wilaya hiyo
kuingia kwenye orodha ya Wilaya zinazochimba Madini ambapo amewataka Wachimbaji
hao kuendelea kuwa watulivu na kufuata Sheria katika uchimbaji wao.
Pia, Waziri Biteko
amesema haki zipo nyingi kuna Haki ya Ardhi, Haki ya Anga, Haki ya Madini na
kadhalika, unaweza ukawa na shamba lakini mmiliki mkuu wa shamba hilo ni
wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenye mamlaka ni Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, kama kwenye shamba hilo kuna Madini hairuhusiwi
yachimbwe mpaka kuwe na leseni katika eneo hilo.
“Yoyote anayepewa leseni
ya Madini kazi yake ya kwanza ni kwenda kwa mwenye shamba sababu huwezi
kuyachimba Madini mpaka ukubaliane na mwenye shamba na kuna makubaliano ya aina
mbili ya kwanza ni kumlipa fidia mwenye shamba ili akupishe na aina ya pili ni
mwenye shamba kuingia shea kwenye leseni husika,” amesema Waziri Biteko.
Pia, Waziri Biteko
amewasisitiza wachimbaji wadogo kuachana na suala la kutorosha madini ambapo
amewataka kuchimba kwa kufuata Sheria na kuhakikisha kodi ya Serikali inalipwa.
“Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anataka kuona Uchumi wa Madini unamilikiwa na Watanzania wa kawaida pia wachimbaji wote walioko sehemu mbalimbali ikiwemo Kaliua wanabadilisha maisha yao kwa rasilimali ambazo Mwenyezi Mungu amewabariki,” amesema Waziri Biteko.
No comments:
Post a Comment