Ndugu Chongolo amesema kuwa ujenzi na kukamilika kwa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 335, ambayo ni kiunganishi muhimu cha mikoa hiyo miwili na mikoa mingine ya Magharibi mwa nchi, ni matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025.
Katibu Mkuu ametoa pongezi hizo leo akiwa njiani kuelekea mkoani Tabora mara baada ya kumaliza ziara ya siku 2 yenye lengo la kuangalia uhai wa chama kuanzia ngazi za mashina na kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.
“Hongereni sana kwa Serikali na Tanroads, kwa maana mmefanya kazi nzuri ya usimamizi, barabara imejengwa kwa kasi nzuri lakini pia mmesimamia thamani ya pesa vizuri,” amesema Katibu Mkuu Ndugu Chongolo”.
Chongolo amesema kukamilika kwa barabara hiyo kuanze kutafsiri uchumi wa wananchi wa maeneo hayo kwani fursa nyingi zitafunguka na ni vyema wakazi wa eneo hilo waanze kula matunda ya barabara hiyo.
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu ameongozana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambao walisimama eneo la Kanono na kujionea hatua za mwisho za ukamilishwaji wa ujenzi wa barabara hiyo ukiendelea ambao umekamilika kwa asilimia 95%.
Kwa upande wake Meneja wa TANROAD mkoa wa Katavi Mhandisi Martin Mwakabende amesema wakati mkoa unaanzishwa ulikuwa na kilomita 1.9 tu za barabara ya kiwango cha lami na mpaka sasa mkoa una kiwango cha kilomita 322 za kiwango cha lami.
Akizungumzia barabara ya Mpanda – Tabora Mkurugenzi huyo wa TANROAD amesema;
“Jumla ya kilomita zinazokwenda kujengwa ni 335 ambazo zimegawanywa katika vipande vitatu, kuna kipande cha kwanza kinaanzia Ususula kuja Komanga kina urefu wa kilomita 108, lakini pia kuna kilomita 9 zimepita kwenye mji wa Sikonge, kipande cha pili kinaanzia Komanga mpaka Kasinde kina kilomita 108 lakini pia kina kilomita 4.2 zimepita katika mji wa Inyonga, na cha tatu kinaanzia Kasinde kuja Mpanda kina kilomita 105. Katika mradi huu Serikali imewekeza kiasi cha bilioni 432.8.”
No comments:
Post a Comment