Monday, October 18, 2021

WAZIRI WA KILIMO MHE. PROF ADOLF MKENDA AWASILI NCHINI BURUNDI KWA ZIARA YA KIKAZI YA SIKU MBILI

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda (Wa Pili Kushoto) akimsikiliza kwa makini mwenyeji wake Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Burundi Bw Salvator Mbilinyi (Wa Kwanza Kulia), mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bujumbura-Burundi leo tarehe 18 Octoba 2021 kwa ajili ya ziara ua kikazi ya siku mbili itakayofanyika tarehe 19-20 Octoba 2021. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Mazao wa Wizara ya Kilimo Bw Enock Nyasebwa (Wa kwanza Kushoto), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania Dkt Stephan Ngailo (Wa Pili Kulia). (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo).

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo, Bujumbura-Burundi


Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda leo tarehe 18 Octoba 2021 amewasili Mjini Bujumbura nchini Burundi kwa ajili ya ziara ua kikazi ya siku mbili itakayofanyika tarehe 19-20 Octoba 2021.


Katika ziara hiyo Waziri Mkenda atakutana na kufanya mazungumzo ya kubadilishana uzoefu na Waziri wa Kilimo wa Burundi kuhusu utekelezaji wa mifumo ya utoaji ruzuku kwenye pembejeo za Kilimo.


Waziri Mkenda pia anatarajiwa kutembelea kiwanda cha Mbolea cha FOMI ambacho kupitia kampuni yake ya ITRACOM imeanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea Jijini Dodoma nchini Tanzania na kujadiliana namna ya kuhakikisha ujenzi na uzalishaji wa kiwanda hicho.


Waziri Mkenda amesema kuwa takribani Asilimia 90 ya mbolea inaagizwa nje ya nchi hivyo mkakati madhubuti wa serikali ya Tanzania ni kuhakikisha mbolea inazalishwa nchini ili kuondokana na utegemezi wa uagizaji wa mbolea nje ya nchi.


Prof Mkenda amesema kuwa Ujenzi wa kiwanda hicho utakapokamilika kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha Tani 600,000 za mbolea ambazo ni Zaidi ya mahitaji ya mbolea nchini Tanzania ambayo ni kati ya Tani 400,000 mpaka Tani 500,000 kwa mwaka.


Amesema kuwa wakati serikali inaendelea na mkakati wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea Tanzania lakini serikali inaendelea na mkakati wa kuhakikisha kuwa inatafuta mbolea inayoweza kupatikana kwa wakati na kuwafikia wakulima kwa bei nafuu.


Kadhalika, Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda atakutana na Taasisi za utafiti wa nchini Burundi zinazoshirikiana na kiwanda cha FOMI katika kufanya tafiti za afya ya udongo na kuibua na kukubaliana maeneo ya ushirikiano katika kilimo kwa lengo la kukuza uchumi baina ya nchi zote mbili.


Katika ziara hiyo Waziri wa Kilimo ameambatana na Mkurugenzi wa Mazao wa Wizara ya Kilimo Bw Enock Nyasebwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania Dkt Stephan Ngailo pamoja na mtaalamu wa udongo Dkt Catherine Senkoro ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Kilimo-TARI Mlingano kilichopo mkoani Tanga.


Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda amepokelewa na Mwenyeji wake Bw Salvatory Mbilinyi ambaye ni Kaimu Balozi katika Ubalozi wa Tanzania nchini Burundi.


MWISHO

No comments:

Post a Comment