Friday, October 8, 2021

WAZIRI LUKUVI AAGIZA WAKUU WA WILAYA KUSIMAMIA UTATUZI WA MIGOGORO YA MIPAKA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akimuelekeza jambo Bibi Asha Mkaku mkazi wa mtaa wa Mwankoko mkoani Singida wakati wa ziara ya timu ya Mawaziri wa Kisekta ilipotembelea mradi wa visima vya maji katika kijiji cha Mwankoko wakati wa ziara ya utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 tarehe 8 Oktoba 2021. Kushoto ni Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi pamoja na viongozi wengine wakimsikiliza mmoja wa wananchi katika kijiji cha Mwankoko aliwasilisha lalamiko la fidia wakati wa ziara ya timu ya Mawaziri wa Kisekta ilipotembelea visima vya maji katika mtaa wa Mwankoko katika ziara ya utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 tarehe 8 Oktoba 2021. 

Moja ya Tanki kwenye mradi wa visima vya maji katika mtaa wa Mwankoko mkoani Singida.

Na Munir Shemweta, WANMM SINGIDA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka Wakuu wa wilaya kuhakikisha wanasimamia na kumaliza migogoro ya ardhi ikiwemo ile ya mipaka ya vijiji kabla ya kuanza zoezi la sensa ya watu na makazi mwezi Agosti 2022.

Akizungumza wakati ziara ya mawaziri wa kisekta katika mkoa wa Singida tarehe 8 Oktoba 2021, Lukuvi alisema  ni aibu kuona hadi sasa kuna migogoro ya  ardhi ikwemo ile ya mipaka kati ya kijiji na kijiji, kata kwa kata na wilaya kwa wilaya wakati wanaopaswa kuishughulikia ni wakuu wa wilaya.

‘’Inakuaje Mkuu wa wilaya aliyepewa nyenzo na Rais anashindwa kushughuilikia migogoro ya mipaka katika vijiji au wilaya na wilaya mpaka waziri aje’’ alihoji Waziri Lukuvi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Wakuu wa Wilaya wanapaswa kusimamia na kumaliza migogoro ya ardhi kwenye maeneo ya mipaka ya vijiji ili wakati wa zoezi la sensa ipatikane takwimu sahihi za idadi ya watu kwenye vijiji.

Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt Binilith Mahenge alisema, ofisi yake sasa itahakikisha inasimamia pamoja na kuifatualia migogoro yote ya ardhi ikiwemo ile ya mipaka katika wilaya na vijiji ili kumaliza kabisa migogoro ya ardhi.

Akielezea utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye mkoa wa Singida, Waziri Lukuvi alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza vijiji 11 kati ya  12 ambavyo wananchi wake wanaishi  katika maeneo ya hifadhi na yale oevu kuendelee kubaki maeneo hayo bila kubughudhiwa.

Hata hivyo, alisema timu ya wataalamu itabaki mkoani Singida kwa ajili ya kufanya tathmini kujua ukubwa wa maeneo yanayotumiwa na wananchi ukiwemo mtaa mmoja katika mkoa huo na kusisitiza kuwa Rais ameamua kumega baadhi ya maeneo na kuwapatia wananchi hivyo hatarajii kuona wakibughudhiwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida Suleiman Mwenda alipongeza hatua iliyochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuamuru wananchi wanaoishi kwenye vijiji vyenye migogoro ya matumizi ya ardhi kubaki na kueleza uamuzi huo utaondoa hofu na taharuki waliyokuwa nayo wakazi wa maeneo hayo kabla ya uamuzi wa serikali.

Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameelekeza Mthamini Mkuu wa Serikali kwenda kufanya uhakiki wa fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa mradi wa visima vya maji katika mtaa wa Mwankoko katika manispaa ya Singida.

Lukuvi alitoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa na serikali kwa ajili ya kupisha ujenzi wa mradi wa visima vya maji katika mtaa wa Mwankoko.

Wananchi  hao wamedai kuwa, zoezi la uthamini wa fidia kwa wananchi wa eneo hilo halikufanyika kwa uwazi kwa kuwa, kumekuwa na ulipwaji uliotafautiana viwango kwa maeneo yanayolingana.

Mmoja wa wananchi wa kitongoji hicho ambaye eneo lake limetwaliwa Bibi Asha Mkaku aliwasilisha lalamiko lake kuwa alilipwa fidia ya sehemu tu ya eneo lake na kumtaka Waziri Lukuvi kusadia ili aweze kupata haki.

‘’ Naagiza Mthamini Mkuu wa Serikali aje hapa afanye kazi hiyo kujua nani anastahili kulipwa kiasi gani na atakapokuja hapa, yule anayeoona hakutendewa haki aje na nyaraka zake zote’’ alisema Lukuvi.

Mwankoko ni eneo lenye hifadhi kubwa ya maji chini ya ardhi ambako visima virefu vimechimbwa kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya maji yanayotimika kwenye mji wa Singida. Eneo hilo lina ukubwa wa ekari 1,653 zilizotwaliwa na serikali kwa kuwalipa fidia wananchi waliokuwepo eneo hilo. Hata hivyo, Baadhi ya wananchi walilalamika kuwa fidia ni ndogo na wengine kulalamika kuwa hawajafanyiwa uthamini.

No comments:

Post a Comment