Thursday, October 7, 2021

WAZAZI NA WALEZI WA WATOTO SHULE YA MSINGI CHUNYA MJINI WAFANIKIWA KUDHITI UKATILII

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akisalimiana na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya alipowasili kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa shughuli za Maendeleo katika ziara yake Mkoani Mbeya.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis,akizungumza na Kamati za ulinzi na usalama wa mama na mtoto ya Kata ya Chalangwa alipotembelea kukagua utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akikagua ujenzi wa Kituo cha Afya katika Mamlaka ya Mji Mdogo Makongolosi Chunya ambapo kikundi Cha wanawake wa nguvu walianzisha ujenzi huo kwa nguvu zao.

Wanakamati wa ulinzi na usalama wa mama na watoto kata ya Chalangwa wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alipotembelea Wilayani hapo kukagua utekelezaji wa Mpango huo.

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Chunya wakimsikiliza Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alipotembelea shuleni hapo kukagua klabu ya watoto ya kupinga ukatili ya TUSEME.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Na Mwandishi Wetu, Chunya

Wazazi na walezi wa watoto wanaosoma katika Shule ya Msingi Chunya mjini, mkoani Mbeya wamefanikiwa kudhibiti ukatili dhidi ya watoto na kupelekea utoro kupungua shuleni na kupanda kwa ufaulu.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alipotembelea Shule ya Msingi Chunya kukagua utendaji wa klabu ya TUSEME iliyoundwa kwa lengo la kutoa elimu kwa watoto kukabiliana na ukatili wa kimwili, kiakili, kingono na kisaikolojia kwa watoto.

Akiwasilisha taarifa kwa niaba ya wanachama wa klabu hiyo, mbele ya Naibu Waziri Mwanaidi Mlezi wa Klabu hiyo mwl. Eliud Dickson amesema Klabu hiyo imewasaidia wazazi na wanafunzi kupungua kwa vitendo vya ukatili kwa kiasi kikubwa ikiwemo mimba, vipigo, ubakaji na hakuna wazazi wanaolalamika watoto wao kufanyiwa ukatili kama ilivyokuwa awali kutokana na elimu inayotolewa.

Ameongeza kuwa Klabu hiyo yenye wanafunzi 100 inahakikisha mtoto anakua na uwezo wa kusema pale anapofanyiwa vitendo vya ukatili na wazazi, walezi, walimu na jamii na kupata malezi bora.

Akizungumza na Wanachama wa klabu hiyo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Chunya kwa kushirikiana na Shirika la UNICEF kuanzisha klabu hiyo iliyochangia kupungua kwa vitendo vya ukatili shuleni hapo na jamii nzima ya Chunya.

“Siku zote tunaambiwa malezi siyo baba na mama tu, mtoto analelewa popote kwenye usalama, hivyo wazazi tuendelee kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya tutaendelea kushirikiana na Wadau wanaoshughulika na masuala ya watoto kuhakikisha ulinzi kwa watoto” amesema Mhe. Mwanaidi.

Akiwa Wilayani Chunya Mhe. Mwanaidi ametembelea kikundi cha wanawake wa nguvu waliochangia nguvu zao katika ujenzi wa Kituo cha Afya katika mji mdogo wa Makongolosi ili kuondoka na changamoto za upatikanaji wa huduma hiyo.

Aidha, amezungumza na Kamati za ulinzi na usalama wa mama na mtoto katika kata ya Chalangwa na kuwataka kuzidi kuwaelimisha wananchi kuripoti vitendo vya ukatili kwa watoto ili Sheria ichukue mkondo wake kutokomeza vitendo vya ukatili.

Naibu Waziri Mwanaidi anaendelea na ziara yake Mkoani Mbeya kwa lengo la kukagua shughuli za Maendeleo na kuamsha Ari kwa wananchi kuchangia nguvu zao katika Maendeleo.

No comments:

Post a Comment