Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisisitiza jambo wakati wa kufunga Mkutano wa Saba wa Wataalam wa Mipangomiji uliofanyika katika hoteli ya Nashera mkoani Morogoro
Sehemu ya wajumbe wa Mkutano wa Saba wa Wataalam wa Mipangomiji wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (Hayupo pichani) wakati wa kufunga mkutano huo katika Hoteli ya Nashera mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji Profesa Wilbard Kombe (Wa tatu Kushoto) pamoja na viongozi wengine wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati wa kufunga mkutano wa Saba wa Wataalam wa Mipangomiji katika Hoteli ya Nashera Morogoro.
Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amewataka Wataalam wa Mipangomiji nchini kuhakikisha wanapopanga mipango yao kwenye maeneo mbalimbali nchini wanatenga maeneo ya wafanyabiashara wa kawaida ili waweze kufanya biashara katika mazingira rafiki na yaliyo bora.
Alisema, baada ya Wataalam hao kutekeleza wajibu wao wa kupanga, halmashauri nchini ambazo ni mamlaka za upangaji ziweke miundombinu ili wafanyanyabiashara hao wapatikane kwenye maeneo maalum yaliyotengwa.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya wafanyabiashara wa kawaida ni sharti yawe na huduma zote muhimu kama vile maji, umeme na barabara ili kuwawezesha kufanya biashara zao hata usiku kwenye maeneo maalum yaliyotengwa.
‘’Mnapoandaa michoro yenu ya mipangomiji zingatieni taaluma huku mkikumbuka kuna makundi maalum kama vile Mamalishe, Machinga, Bodaboda na watanzania wa kawaida na muwawekee utaratibu maalum wa kupata ardhi kwa gharama nafuu ili nao waweze kushiriki kujenga maeneo yaliyopangwa’’ alisema Naibu Waziri Dkt Mabula
Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano Mkuu wa Saba wa Wataalamu wa Mipangomiji uliofanyika tarehe 27 Oktoba 2021 mkoani Morogoro, Naibu Waziri Mabula alisema, mipango ya uendelezaji miji na michoro ya mipangomiji inapoandaliwa ipelekwe mitaani katika lugha ambayo wana mitaa wanaweza kuielewa.
‘’Mipango ya uendelezaji miji inapoandaliwa iletwe mitaani katika lugha ambayo wana mitaa wanaweza kuielewa ili waweze kusimamia, sababu wao ndiyo wadau na watasaidia hata katika development control’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha, aliwataka Wataalam wa Mipangomiji kushirikisha watendaji kata, mitaa na vijiji katika mipango ya uendelezaji mji kwa kuwa wao ndiyo wadau muhimu na kusisitiza kuwa wadau hao ni nguvu kazi itakayosaidia kupunguza ujenzi holela kwenye maeneo ya mijini na vijijini.
Naibu Waziri wa Ardhi aliwaasa Wataalam Mipangomiji kuwa wabunifu na kuandaa miradi shirikishi isiyokuwa na suala la fidia na kubainisha kuwa miradi hiyo ni lazima itafanikiwa kwa kuwa itakuwa imeshirikisha wananchi watakaojiona kama sehemu ya wamiliki wa miradi hiyo.
Pia aliitaka Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji kuendelea kusimamia nidhamu, maadili na uwajibikaji kwa wataalamu wa sekta hiyo ili kuleta ufanisi katika sekta ya mipangomiji.
Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipangomiji Profesa Wilbard Kombe alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi kuwa, katika maazimio yake wajumbe wa mkutano huo walipendekeza kufanyika mabadiliko kwenye sheria namba nne kwenye kifungu kinachohusu mfuko wa fidia ili watumiaji wakubwa wa ardhi wachangie mfuko huo.
‘’Tumeona huu ni wakati muafaka kwa watumiaji wakubwa wakachangia katika huu mfuko ili kuipa nguvu wizara kumudu gharama zinazotokana na fidia hasa baada ya ardhi kuwa na thamani, kutegemea wizara moja kumudu jukumu hili ni ngumu sana hivyo tumeona ni wakati muafaka kufanya mabadiliko kwenye sheria hiyo’’ alisema Kombe.
Mkutano huo wa Wataalam wa Mipangomiji nchini wenye kauli mbiu ‘Mipangomiji na Uwekezaji Shirikishi Tanzania’ ulishirikisha Wataalamu wa Mipangomiji 230 kutoka mikoa mbalimbali nchini na ulifunguliwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.
No comments:
Post a Comment