Wednesday, October 13, 2021

Makamu wa Rais apongeza utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango amekagua utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na kupongeza hatua za ujenzi  zilizofikiwa. 

Ametoa pongezi hizo tarehe 12 Oktoba, 2021 wakati akitembelea maeneo mbalimbali ya mradi huo unaotekelezwa katika mkoa wa Pwani na Morogoro akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati na Mikoa ya Pwani na Morogoro wakiongozwa na Waziri wa Nishati, January Makamba. 

Maeneo aliyotembelea ni pamoja na ujenzi waTuta kuu la Bwawa, Njia za kupeleka maji kwenye mitambo itakayofua umeme, Jengo la mitambo pamoja na ujenzi wa kituo cha kupokea na kusafirisha umeme. 

“Mheshimiwa Waziri wa Nishati pamoja na TANESCO nawapongeza kwa kuendelea kusimamia ujenzi wa mradi huu, mnafanya kazi nzuri sana, Serikali inawapongeza na jicho la Serikali liko hapa kwani tuliwaahidi Watanzania kwamba tutaujenga mradi huu ili tupate umeme wa kutosha utakaojenga uchumi wa viwanda,” alisema Makamu wa Rais 

Aliwataka viongozi hao kuendelea kuchapa kazi, kutanguliza uzalendo na kuwa makini ili kuhakikisha kwamba mradi huo unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa. 

Akiwa kwenye eneo unakoendelea ujenzi wa Tuta kuu la bwawa, Makamu wa Rais aliwaelekeza wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha kuwa kila kitu kinatekelezwa kwa umakini mkubwa ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea endapo mradi huo utaanza kufanya kazi huku ukiwa na mapungufu. 

“Ninyi kama wasimamizi wa mradi, mhakikishe kwamba kama kuna hitilafu inaonekana ifuatiliwe kwa ukamilifu, ikitokea tatizo lolote la kiufundi na hili bwawa likapasuka hapo baadaye madhara huko mbele yatakuwa makubwa, hatutaki kuingiza nchi yetu kwenye historia mbaya,” alisisitiza Makamu wa Rais 

Aliongeza kuwa, taratibu zote za kitalaam zifuatiliwe na vigezo vizingatiwe kwa asilimia 100 na hata kama kuna hitilafu ndogo ifutiliwe chanzo chake kwa maslahi mapana ya nchi. 

Alitaja gharama za utekelezaji wa mradi huo ni shilingi Trilioni 6.5 na kuwaasa watanzania kuendelea kulipa kodi ambayo ndiyo inayotekeleza miradi mikubwa kama huo wa bwawa la Julius Nyerere. 

Kwa upande wa mazingira amaeagiza kuwa kuwe na usimamizi mkubwa wa masuala yote yatakayoathiri ujazaji maji katika bwawa hilo ili ndoto ya kuzalisha umeme katika bwawa hilo itimie. 

“Siyo tujenge tu bwawa zuri lakini tukaja hapo baadae tukaliharibu, hivyo nawaombeni wakuu wa Mikoa, Wabunge na Wakuu wa Wilaya kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhakikisha kwamba mazingira ya maeneo yanayohusu mradi huo yanabaki salama na safi ili bwawa litupatie kile tunachokitaka kama vile umeme, uvuvi na umwagiliaji na utalii,” alisema Makamu wa Rais. 

Awali, Waziri wa Nishati, January Makamba, alimshukuru Makamu wa Rais kuwa, kwa kutembelea mradi huo kwani inaonesha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inatoa uzito na kuupa umuhimu mradi huo wa JNHPP. 

Alisema kuwa, Wizara ya Nishati pamoja na TANESCO wanafahamu dhamana kubwa waliyokabidhiwa na nchi katika kusimamia mradi huo ambao una maana kubwa kwa Taifa na ni ishara na kielelezo cha maono makubwa ambayo viongozi wamekuwa nayo, kielelezo cha Taifa linalotaka kupiga hatua mbele na pia ni kielelezo cha kusukuma maendeleo na kuwajali wananchi 

Alieleza kuwa, Wizara ya Nishati pamoja TANESCO wanachukulia dhamana hiyo  kwa uzito mkubwa na heshima kubwa hivyo ahadi wanayoitoa ni kutimiza wajibu kwa uadilifu na weledi ili kutowaangusha Viongozi wa Nchi na watanzania kwa ujumla. 

Viongozi wa Wizara ya Nishati walioambatana na Makamu wa Rais katika ziara hiyo ni  Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Felchesmi Mramba na Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment