Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Oktoba 7, 2021 amekataa kufungua barabara yenye uefu wa kilimia 1.2 iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Liwale mkoani Lindi ambayo ujenzi wake haujakamilika kwa mujibu wa mkataba ulitiwa saini kati ya mkadarasi na Serikali. Wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Kasekenya, wa pili kulia ni Mbunge wa Liwale, Kuchauka na kulia ni Meneja wa TANROADS mkoa wa Lindi Mlavi Efatha (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokataa kufungua barabara yenye uefu wa kilimia 1.2 iliyopo katika halmashauri ya wilaya ya Liwale mkoani Lindi ambayo ujenzi wake haujakamilika kwa mujibu wa mkataba uliotiwa saini kati ya mkadarasi na Serikali. Wa tatu kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, wa pili kulia ni Mbunge wa Liwale, Zuberi Kuchauka na kulia ni Meneja wa TANROADS mkoa wa Lindi Mlavi Efatha(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Muonekano wa barabara yenye urefu wa kilomita 1.2 ambayo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikataa kuifungua baada ya kubainika kuwa ujenzi wake haujakamilika kwa mujibu wa mkataba wa ujenzi wake uliotiwa saini kati na mkandarasi na Serikali. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimia Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara ya kutoka Nangurukuru hadi Liwale yenye urefu wa kilomita 231 ikiwa ni maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami.
Pia, Mheshimiwa Majaliwa amegoma kufungua barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 1.2 iliyoko katika halmashauri ya wilaya ya Liwale mkoani Lindi kwa sababu ujenzi wake haujakamilika ikiwemo kuwekwa taa za barabarani kama mkataba wa ujenzi wake unavyoelekeza.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 7, 2021) wakati akizungumza na wananchi katika eneo la Idara ya Maji Kata ya Liwale Mjini ambapo palitengwa kwa ajili ya ufunguzi wa barabara hiyo akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Lindi.
“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kila panapojengwa barabara na ikiwa inapita kwenye eneo la mji basi pawekwe na taa sasa hapa taa hakuna, hivyo barabara hii haijakamilika kwa hiyo siifungui naomba nikazungumze mengine pale na wananchi.”
Naye, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo barabara ya kutoka Nangurukuru hadi Liwale ikiwa ni pamoja na kujenga makaravati ili kuiwezesha kupitika wakati wote.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Halmashauri ya wilaya ya Kilwa na Liwale wamemshukuru Mheshimiwa Rais Samia kwa uamuzi wake wa kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami kwa sababu itakapokamilika itachochea ukuaji wa uchumi na kwa kurahisisha shughuli za usafiri.
Mapema leo akiwa njiani kuelekea wilayani Liwale, Waziri Mkuu alizungumza na wananchi katika kijiji cha Kipindimbi na Zinga Kibaoni wilayani Kilwa ambapo amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha huduma za kijamii zikiwemo za Afya, Maji, Elimu, Umeme na Mawasiliano zinapatikana maeneo yote nchini.
Akizungumzia kuhusu Elimu, Waziri Mkuu ameuagiza ugozi wa wa wilaya ya Kilwa uhakikishe kuwa kati ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu katika halmashauri hiyo uhakikishe kijiji cha Kipindimbi kinapewa kipaumbele kwa kuboreshewa miundombinu na kuongezewa vyumba vya madarasa katika shule yao ya msingi.
Pia, Waziri Mkuu amewataka wazazi wahakikishe watoto wote wenye umri wa kwenda shule wakiwemo watoto wa kike wanapelekwa kwani Serikali imeondoa michango iliyokuwa inakwaza wananchi.
“Wala usifikirie kuoa wala kumpa ujauzito mwanafunzi kwa sababu Serikali imeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike na ukibainika umempa ujauzito au kumkatisha masomo adhabu yake ni jela miaka 30. Tuhakikishe tunawatunza, tunawalinda na kuwasaidia mtoto wa kike ili watimize ndoto zao kielimu”
Pia, Waziri Mkuu ametoa maagizo kwa viongozi wa vijiji hususani katika maeneo ya wafugaji kwamba wahakikishe watoto wote wanakwenda shule na wawakamate na kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wote wanaowapa watoto kazi ya kuchunga mifugo badala ya kwenda shule.
Akizungumza kuhusu changamoto ya mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itaendelea kushirikiana na kampuni mbalimbali za mawasiliano ili kufikisha huduma hiyo katika maeneo yote hivyo amewataka wananchi waendelee kuwa na matumaini na Serikali yao.
Kadhalika, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kilwa uhakikishe kata ya Kipindimbi inawekwa kwenye mpango wa kujengewa kituo cha afya. “Mheshimiwa Rais Samia ametoa pesa kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya kwenye maeneo yote yenye uhitaji, niwahakikishie kwamba hapa Kipindimbi tutajenga kituo cha afya ili kusogeza huduma kwa wananchi”
Vilevile, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuchoma misitu na badala yake wailinde maliasili hiyo ili iweze kuwanufaisha Watanzania wote. “tunahitaji maji, tukichoma misitu hii hatuwezi kupata maji kwa kuwa tutaharibu vyanzo na kusababisha Taifa kugeuka jangwa”.
No comments:
Post a Comment