Naibu Waziri Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa David Silinde akizungumza katika moja ya mikutano ya Mawaziri wa Kisekta kutoa mrejesho wa utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji.
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Tabora Hassan Wakasuvi akizungumza katika mkutano wa Mawaziri wa Kisekta kutoa mrejesho maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji mkoa wa Tabora.
Wananchi wa kijiji cha Kigwa wilayani Uyui mkoani Tabora wakifurahia uamuzi wa kijiji hicho kumegewa sehemu ya ardhi ya Hifadhi ya Kigwa-Rubuga wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.
Sehemu ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta wakiwa katika mkutano wa wananchi katika kijiji cha Kigwa wilayani Uyui mkoa wa Tabora. Wa nnne kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Tabora Dkt Batilda Burian.
Munir Shemweta WANMM TABORA
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) David Silinde amesema kuanzia sasa ofisi yake haitasajili vijiji bila kushirikisha wadau muhimu ili kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi inayojitokeza
Hatua hiyo ni kutaka kuondoa mgongano uliojitokeza wakati wa kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975 ambapo ilibainika baadhi ya vijiji kusajiliwa ndani ya mipaka ya hifadhi.
‘’Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza TAMISEMI iwe inashirikisha wadau muhimu wakati wa kusajili vijiji ili kuondokana na migogoro ya matumizi ya ardhi iliyojitokeza kwenye vijiji 975’’ alisema Silinde.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri TAMISEMI, wakati Kamati ya Mawaziri nane ikishughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi, baadhi ya vijiji vimeonekana kuwa ndani ya hifadhi na wananchi wake wamekuwa wakishiriki chaguzi mbalimbali zikiwemo zile za za serikali za mitaa.
Wadau muhimu watakaoshirikishwa katika usajili wa vijiji ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Ulinzi pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii.
‘’Ofisi ya rais TAMISEMI ndiyo inayohusika na usajili wa vijiji lakini kutokana na matatizo yaliyojitokeza kwenye migogoro hii ya vijiji 975 kuanzia sasa hatutasajili tena kijiji mpaka tuwasiliane na sekta nyingine kama vile Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Wizara ya Ulinzi’’ alisema Silinde.
Akizungumza mkoani Tabora tarehe 12 Oktoba 2021 Silinde alisema, kutoshirikisha wadau muhimu wakati wa kusajili vijiji kumesababisha kuwepo vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi na hivyo kuchangia migogoro ya matumizi ya ardhi.
Wakati wa kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 Kamati ya Mwaziri inayoongozwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ilibaini baadhi ya vijiji kusajiliwa ndani ya mipaka ya hifadhi na kuwa na miundombinu ya kijamii.
Akielezea utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema, mkoa wa Tabora unahusisha vijiji 100 na ni mkoa wenye vijiji vingi ukilinganisha na mikoa mingine ambapo vijiji 94 kati ya hivyo ndivyo vitakavyobaki na maeneo yake kama yalivyo.
Kwa mujibu wa Lukuvi, mchanganuo wa utekelezaji maamuzi Baraza la Mawaziri ni kuwa vijiji 50 vilivyosajiliwa ndani ya hifadhi vitaendelea na hadhi yake huku vijiji 15 migogoro yake ikiwa tayari imetatuliwa na kijiji kimoja vitongoji vyake vitabaki kwenye hifadhi .
Aidha, alisema kuna vijiji 11 vitakavyomegewa maeneo katika hifadhi na vijiji 17 vilivyokuwa na migogoro ya mipaka na hifadhi vitabaki lakini mipaka yake itarejewa kwa njia shirikishi.
‘’Rais wa Jamhuri ya ,Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametuelekeza tutekeleze uamuzi huu kwa umakini mkubwa bila ya kuleta taharuki kwa wananchi na kwa kuzingatia maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla’’ alisema Lukuvi.
No comments:
Post a Comment