Monday, September 27, 2021

WAZIRI BITEKO AMPONGEZA RMO FABIAN KWA USIMAMIZI MZURI WA TANZANITE

Na Mwandishi wetu, Mirerani

WAZIRI wa madini Dotto Biteko amempongeza Ofisa madini Mkazi (RMO) wa Mirerani, Fabian Mshai kwa namna anavyousimamia ipasavyo Mkoa wa kimadini wa Simanjiro kwa kutatua kero za wadau wa madini.

Biteko akizungumza na wadau wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani ameeleza kuwa amepata taarifa kwa kupitia watu mbalimbali kuwa RMO Fabian anafanya kazi hiyo kwa ueledi mkubwa.

“Nataka nimpe moyo msaidizi wangu RMO Fabian Mshai kwa namna wadau wa madini wanavyokupongeza unavyochapa kazi endelea hivyo hivyo,” amesema Biteko.

Amesema hivi karibuni wanawake wa biashara ya magonga walikuwa wanalia juu ya kubanwa kwenye kazi yao na wakamtuma Mbunge wa Jimbo hilo Christopher Ole Sendeka akawasiliana naye wakalitatua.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Christopher Ole Sendeka amesema RMO Fabian Mshai anastahili pongezi kwani kilio cha wanawake wa magonga walipokuwa wanazuiwa kuyongeza thamani alitatua kero hiyo mara moja.

“Wanawake wa magonga wa madini ya Tanzanite wamenituma nifikishe shukrani zao kwako Waziri Biteko kwani RMO Fabian ametatua changamoto zao na sasa wanafanya shughuli zao za kujikimu kimaisha bila tatizo lolote,” amesema Ole Sendeka.

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani Adam Kobelo amesema RMO Fabian Mshai ni kijana mchapakazi mwenye kusikiliza wadau wa madini na mwenye kupokea ushauri.

“RMO Fabian anafahamu maana ya uongozi kwani wadau wa madini wakileta changamoto zao kwetu sisi tukizipeleka kwake anazitatua,” amesema Kobelo.

No comments:

Post a Comment