Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akitoa maelezo kuhusu Azimio la Bunge kuhusu Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango Vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula (East African Community Protocol on Sanitary and Phytosanitary Measures – EAC SPS), Bungeni Jijini Dodoma Leo tarehe 8 Septemba 2021. (Picha Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
1.0
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, Ninapenda kutoa hoja kwamba Bunge lako tukufu lijadili
na kukubali kupitisha Azimio la Bunge kuhusu Itifaki ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki ya Viwango Vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula (East African Community Protocol on Sanitary and Phytosanitary Measures
– EAC SPS)
Mheshimiwa
Spika, Chimbuko la Azimio la Kuridhia Itifaki ya EAC- SPS ni
Ibara ya 151 ya Mkataba wa EAC inayoeleza
kuwa nchi wanachama zitaandaa Itifaki (Protocols) katika maeneo yote ya
ushirikiano pale inapobidi. Vilevile, Ibara za 105 hadi 110 za Mkataba huo zinataka
nchi wanachama kushirikiana katika Sekta ya Kilimo na Chakula ambapo kwa upande
wa Viwango vya SPS inataka nchi hizo
kudhibiti magonjwa ya mimea na wanyama; kuwianisha Sera, Sheria na Kanuni za kudhibiti
visumbufu na magonjwa; kuwianisha na kuimarisha taasisi za usimamizi na
kuwianisha na kuimarisha huduma za ukaguzi na utoaji wa vyeti kwa ajili ya
usafi mimea (Phytosanitary) na wanyama au bidhaa za wanyama (zoo-sanitary). Aidha, Itifaki ya Umoja wa Forodha (Customs Union) inataka ushirikiano katika eneo hili ili kukuza
biashara ndani na nje ya EAC.
Mheshimiwa
Spika, nchi wanachama wa EAC
ziliandaa Itifaki ya SPS ikiwa ni utekelezaji wa Ibara ya 151 ili kuwianisha
viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula.
Aidha, Itifaki hiyo ilisainiwa na Baraza la Sekta ya
Kilimo na Usalama wa Chakula tarehe 12 Julai 2013 Jijini, Arusha na baadaye
kuidhinishwa na Wakuu wa nchi wanachama katika Mkutano Mkuu wa 14.
2.0
WARAKA WA MAPENDEKEZO YA KURIDHIA ITIFAKI
Mheshimiwa
Spika, Wizara ya Kilimo
iliandaa Waraka wa Mapendekezo ya kuridhia Itifaki ya EAC SPS kwa kuhusisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara mbalimbali zikiwemo Fedha na Mipango, Sheria na Katiba,
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Mifugo na Uvuvi, Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na
Watoto, Viwanda na Biashara, Maliasili na Utalii. Wadau wengine ni Ofisi ya
Makamu wa Rais Mazingira, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la
Viwango Tanzania (TBS), Taasisi ya Uthibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI),
Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu Ukanda wa Kitropiki (TPRI),
Taasisi Kilele ya Mazao ya Bustani (TAHA), Ofisi ya Hifadhi ya Mimea Zanzibar, Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Tume ya Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Spika, Waraka Na. 34/2013-14 wa Mapendekezo ya Kuridhia Itifaki ya EAC SPS uliwasilishwa kwenye Kikao cha Baraza la Mawaziri cha tarehe 03 Juni, 2015 ambapo Baraza liliagiza kuwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iandae Azimio la Bunge kwa ajili ya Kuiridhia Itifaki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (The East African Cummunity Protocol on Sanitary and Phytosanitary Measures) na kuliwasilisha Bungeni ili liweze kuridhiwa ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, kabla ya hatua hii ya kuridhiwa kwa Itifaki Serikali kwa
kushirikiana na wadau wa sekta binafsi imefanya majadiliano ya kina kwa kupitia
maeneo yote yanayohusu Itifaki kwa lengo la kuwa na uelewa wa pamoja na
kuainisha mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa utekelezaji wa Itifaki ili
kulinda na kutetea maslahi ya Tanzania.
3.0
MADHUMUNI YA ITIFAKI YA EAC -SPS
Mheshimiwa
Spika, Madhumuni ya Itifaki yaliyoainishwa
katika Ibara ya 2 ni yafuatayo:-
(a) Kukuza biashara ya chakula na bidhaa za kilimo ndani na nje ya Jumuiya;
(b)
Kuhimiza utekelezaji wa Misingi Mikuu ya Makubaliano
ya Matumizi ya Viwango vya SPS (the WTO
Agreement on the Application of Sanitary and Phytosanitary Measures) (uwianishaji
(harmonisation), equivalence, regionalisation, transparency (uwazi) na
tathmini ya athari (risk assessment);
(c) Kuimarisha ushirikiano na uratibu wa viwango na shughuli
za Afya ya Mimea, Wanyama na usalama wa chakula kitaifa na kikanda kwa
kuzingatia uelewa wa pamoja matumizi ya viwango hivyo ndani ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki; na
(d)
Kuimarisha
hadhi ya viwango vya SPS kwa kuzingatia vigezo vya kisayansi ndani ya Jumuiya.
4.0
IBARA ZA ITIFAKI NA MAUDHUI YAKE
Mheshimiwa
Spika, Itifaki ina Ibara 17.
Nitataja baadhi ya Ibara hizo na maudhui yake kwa ufupi ifuatavyo :-
Ibara
ya 2 inahusu madhumuni ya
Itifaki kama nilivyoeleza katika sehemu ya 3.0 hapo juu.
Ibara
ya 3 inaeleza kuwa mawanda ya ushirikiano ni katika
kutumia (adoption) viwango vya SPS kwa kuwianisha viwango vya afya ya mimea,
wanyama na usalama wa chakula;
Ibara
ya 4 hadi 6 zinazungumzia
ushirikiano katika masuala yanayohusu afya ya mimea, wanyama na usalama wa
chakula na hatua mbalimbali ambazo nchi wanachama zinapaswa kutekeleza kupitia
ushirikiano huo;
Ibara
ya 7 inahusu nchi wanachama
kuteua Mamlaka na/au Taasisi mahiri (competent authorities) kwa madhumuni ya
Itifaki.
Ibara
ya 8 inahusu udhibiti na
uwezeshaji wa biashara ya chakula na bidhaa za kilimo kwenye vituo vya
mipakani.
Ibara
ya 9 inaeleza nchi wanachama
zitashirikiana katika kubadilishana taarifa na utaalam kuhusu viwango vya afya
ya mimea, wanyama na usalama wa chakula kupitia uanzishwaji na uendeshaji wa
mfumo wa kikanda kuhusiana na madhumuni ya Itifaki.
Ibara
ya 10 inahusu ushirikiano
katika kutafuta msaada wa kiufundi ili
kujenga uwezo wa nchi wanachama katika kutekeleza viwango vya SPS;
Ibara
ya 11 inahusu nchi wanachama kuwianisha
Sera, Sheria, kanuni na Programu ili kufanikisha madhumuni ya itifaki;
Ibara
ya 12 inahusu mfumo wa
kitaasisi ambapo Baraza la Mawaziri lililoanzishwa kwa mujibu wa Ubara ya Tisa
(9) ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wenye
dhamana ya ushirikiano wa Afrika Mashariki litaanzisha taasisi zitakazopewa
mamlaka ya kutekeleza madhumuni ya Itifaki kwa kadri itakavyoonekana inafaa;
Ibara ya 13 inahusu mamlaka ya Baraza katika kutunga Kanuni, kutoa maelekezo na kufanya maamuzi kwa kadri itakavyoonekana inafaa kwa mujibu wa madhumuni ya Itifaki hii.
Ibara
ya 14 kinafafanua kwamba
Usuluhishi wa Mgogogoro (Dispute
settlement) kati ya nchi wanachama kuhusu tafsiri au utekelezaji wa Itifaki
utatatuliwa kwa mujibu wa MKATABA wa Jumuiya ya EAC;
Ibara
ya 15 inatoa fursa kwa nchi
wanachama kuifanyia marekebisho Itifaki hii kwa kuzingatia Ibara ya 150 ya
Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ibara
ya 16 cha inaeleza kuwa
Itifaki itaanza kutumika baada ya kuridhiwa na nchi zote wanachama wa Jumuiya.
Ibara
ya 17 inaeleza kuwa Itifaki hii
na nyaraka zote za kuiridhia zitawasilishwa kwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki ambaye atarejesha nakala kwa nchi wanachama. Aidha, Itifaki
itasajiliwa katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa zenye jukumu la kutekeleza viwango
vya SPS.
5.0
AZIMIO LA BUNGE LA KURIDHIA ITIFAKI YA EAC -SPS
Mheshimiwa
Spika, Kwa mujibu wa Ibara ya 16 ya Itifaki, nchi wanachama
zinatakiwa kuiridhia Itifaki hii kwa kuzingatia taratibu za nchi husika. Aidha,
Ibara ya 17 inataka nchi wanachama zilizoridhia Itifaki kuwasilisha kwa Katibu
Mkuu wa Jumuiya Maazimio (instruments of ratification) ya Kuridhia Itifaki hii.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepewa mamlaka
ya kuridhia Itifaki hii kwa mujibu wa Ibara ya 63 (3) (e) ya Katiba ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
6.0
MATOKEO NA FAIDA ZA KURIDHIA ITIFAKI
Mheshimiwa
Spika, Tanzania kwa kuridhia Itifaki hii itaimarisha na
kuboresha afya na usafi wa mimea, wanyama na usalama wa chakula. Utekelezaji wa
Itifaki hii utaharakisha maendeleo katika Sekta ya Kilimo; ubora wa mazao,
usalama wa chakula na kukua kwa biashara. Baadhi ya matokeo yatakayotokana na
kuridhiwa kwa Itifaki hii ni pamoja na:
i.
Kukua
kwa biashara ya chakula na mazao ya kilimo miongoni mwa nchi wanachama wa
Jumuiya na hivyo kuongezeka kwa fursa ya bidhaa zetu kuingia kwenye soko la
Jumuiya bila vikwazo ikiwa ni matokeo ya ulinganifu wa viwango vya afya ya
mimea, wanyama na usalama wa chakula;
ii.
Itatoa
fursa za kuimarisha ushirikiano katika kujenga uwezo wa wataalam na utafiti
unaolenga viwango vya afya ya mimea, wanyama na usalama wa chakula;
iii.
Kuwezesha
nchi yetu kuwa na nguvu ya pamoja na nchi nyingine katika kutetea bidhaa
zinazosafirishwa kutoka ndani ya Jumuiya kuingia katika soko la kimataifa;
iv.
Kuimarisha
uratibu kwa kuwa na Mwongozo wa pamoja ndani ya Jumuiya kuhusu afya ya mimea,
wanyama na usalama wa chakula;
v.
Kuwepo
kwa fursa ya pamoja katika Kanda ya kujilinda dhidi ya magonjwa na visumbufu
vya mimea na wanyama;
vi.
Kuboresha
afya na usafi wa mimea, wanyama na usalama wa chakula na hivyo kuimarika kwa
maisha ya wananchi katika nchi wanachama;
vii.
Kuongezeka
kwa hamasa miongoni mwa wakulima, wafugaji, taasisi na wafanyabiashara wa
chakula na mazao ya kilimo katika kuongeza viwango vya ubora wa bidhaa na
huduma kwa kuzingatia misingi ya kitaalamu na kisayansi ili kukidhi viwango vya
afya ya mimea, wanyama na usalama wa Chakula;
viii.
Kupungua
kwa vikwazo visivyo vya kiforodha mipakani vinavyohusu biashara ya mazao ya kilimo,
mifugo na uvuvi kutokana na Uwazi na tathmini ya athari kulingana na
makubaliano yanayohusu masuala ya viwango vya afya ya mimea, manyama na
chakula;
ix.
Kuoanisha
taratibu za uthibiti na ukaguzi wa mazao mipakani zitakazoondoa matakwa yasiyo
ya lazima yanayoambatana na milolongo mirefu ya taratibu; na
x.
Kuimarisha
utengamano wa kikanda (regionalization integration);
7.0
MAMBO YA KUZINGATIA KATIKA UTEKELEZAJI WA ITIFAKI
Mheshimiwa
Spika, wakati wa utekelezaji
wa Itifaki hii Serikali itahakikisha kuwa
i. Uwianishaji wa Sera, Sheria na Kanuni kwa mujibu wa
Itifaki hii unazingatia maslahi ya nchi na Jumuiya kwa ujumla ambapo tahadhari
dhidi ya uingizaji wa mazao na bidhaa zilizobadilishwa vinasaba
(GMOs) zitaendelea kuchukuliwa kwa kuzingatia Sheria za
Tanzania. Aidha, Tanzania itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba Jumuiya ya
Afrika Mashariki haitumiki kama eneo la kuingiza bidhaa na mazao ya kilimo,
mifugo na uvuvi zinazoweza kuhatarisha usalama wa chakula, usalama wa nchi,
wanyama na mazingira.
ii. Baada ya kuridhiwa kwa Itifaki, Serikali itaendelea
kuzijengea uwezo taasisi zote zinazohusika na utekelezaji wa Itifaki hii
hususan uwezo wa wataalam, utafiti, miundombinu, vifaa na vitendea kazi.
iii. Mpango wa kutoa elimu utawekwa kwa ajili ya kutoa elimu
kwa umma kupitia vyombo vya habari kama vile radio, luninga, vipeperushi na
magazeti.
Pia elimu itatolewa kupitia mitandao ya kijamii,
uchapishaji wa majalada na tovuti za Serikali.
8.0 Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo
hayo, sasa naomba kuwasilisha Azimio hili kwa mujibu wa Ibara ya 63(3)(e) ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ifuatavyo:-
Prof. Adolf F.
Mkenda (Mb.)
WAZIRI
WA KILIMO
No comments:
Post a Comment