Waziri wa Nishati,
Dkt.Medard Kalemani akizungumza na wananchi katika mtaa wa Kyangu (Hawapo
pichani) wakati wa hafla ya kuzindua matumizi ya Gesi Asilia katika nyumba 300
wilayani Mtwara.
Naibu Waziri wa
Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza na wananchi katika mtaa wa Kyangu
(Hawapo pichani) wakati wa hafla ya kuzindua matumizi ya Gesi Asilia katika nyumba
300 wilayani Mtwara tarehe 25 Agosti, 2021.
Mkuu wa Wilaya ya
Mtwara, Dunstan Kyobya akizungumza na wananchi katika mtaa wa Kyangu (Hawapo
pichani) wakati wa hafla ya kuzindua matumizi ya Gesi Asilia katika nyumba 300
wilayani Mtwara tarehe 25 Agosti, 2021.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Meya wa Manispaa ya Mtwara, Shadida Ndile, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Khalfan Khalfan wakiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Kampuni ya usambazaji Gesi (GASCO) mara baada ya kuzindua matumizi ya Gesi Asilia katika nyumba 300 wilayani Mtwara tarehe 25 Agosti, 2021. Nyuma ya Waziri wa Nishati ni Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, James Mataragio.
Waziri wa Nishati, Dkt.Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, wakikata utepe katika nyumba ya Bi. Magreth James, ikiwa ni ishara ya kuzindua matumizi ya Gesi Asilia katika nyumba 300 wilayani Mtwara tarehe 25 Agosti, 2021.
Na Teresia Mhagama
Waziri wa Nishati,
Dkt. Medard Kalemani amezindua matumizi ya Gesi Asilia majumbani katika nyumba
300 ambazo zimeunganishwa na nishati hiyo wilayani Mtwara kwa gharama ya
shilingi milioni 961.7
Uzinduzi huo
ulifanyika tarehe 25 Agosti, 2021 katika Mtaa wa Kyangu wilayani Mtwara, na
kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Viongozi
mbalimbali katika Mkoa wa Mtwara wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara,
Dunstan Kyobya, Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Adam Zuberi,
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Khalfan
Khalfan, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt.James Mataragio na Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje.
“ Hii ni awamu ya Pili
ya usambazaji Gesi Asilia majumbani katika Mkoa wa Mtwara kwani katika awamu ya
kwanza wateja takriban 125 waliunganishwa na wananufaika na gesi hii katika
mitaa ya Reli A na B, Kyangu, Masandube na Lilungu.” Alisema Dkt.Kalemani
Ili kuhakikisha
nishati hiyo inawafikia wananchi wengi zaidi, aliiagiza TPDC na kampuni yake
tanzu inayohusika na usambazaji wa Gesi Asilia (GASCO), kusambaza gesi hiyo kwa
wananchi wote bila kubagua kutokana na manufaa yake mbalimbali kama vile unafuu
wa gharama kulinganisha na nishati nyingine zinazotumika kupikia, pia
inapunguza uharibifu wa mazingira.
Aidha, alieleza kuwa
matumizi ya Gesi Asilia mkoani humo yasiishie tu kwenye Taasisi na majumbani,
hivyo ameiagiza TPDC kufungua kituo cha kujazia gesi kwenye magari na kwenye
viwanda mbalimbali.
Vilevile, Waziri wa
Nishati aliiagiza TPDC, kuendelea kutumia vifaa vinavyotengenezwa
ndani ya nchi katika shughuli za usambazaji Gesi Asilia majumbani na
kueleza kwa kufanya hivyo kutaleta manufaa mbalimbali ikiwemo kuongezeka kwa
ajira na uhakika wa upatikanaji wa vifaa.
Aliongeza kuwa lengo
la Serikali sasa ni kupeleka Gesi Asilia hadi vijijini kupitia mpango wa
usambazaji nishati vijijini, hivyo aliwaagiza TPDC kuendelea kuwahamasisha
wananchi kutumia nishati hiyo.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya
Sita itahakikisha kwa Gesi Asilia iliyopo inawanufaisha wananchi mkoani Mtwara
na watanzania kwa ujumla.
Kuhusu maagizo
mbalimbali yaliyotolewa na Waziri wa Nishati, alieleza kuwa atahakikisha
yanatekelezwa kwa ufanisi kwa kushirikiana na Taasisi zilizo chini ya Wizara
zinazohusika na nishati hiyo.
Awali Mkurugenzi
Mtendaji wa TPDC, James Mataragio alisema kuwa kazi ya usambazaji Gesi Asilia
majumbani ni endelevu kwani katika mwaka 2021/22 Serikali imetenga fedha kwa
ajili ya kuunganisha nishati hiyo katika nyumba nyingine 300.
Kuhusu mradi wa
usambazaji Gesi Asilia majumbani wa Awamu ya Pili, alieleza kuwa umetekelezwa
na wataalam wa ndani ambao ni wahandisi watanzania kutoka kampuni ya GASCO
tofauti na mradi wa Awamu ya kwanza ambao ulitumia wakandarasi na hivyo gharama
zake zilikuwa juu tofauti na mradi wa Awamu ya Pili.
Alifafanua kuwa, mradi
wa Awamu ya Kwanza ulitumia katribani shilingi Bilioni 3.2 huku mradi wa Awamu
ya Pili ukitumia shilingi milioni 961.7 hivyo Serikali imeokoa fedha takriban
shilingi Bilioni 2.
Alisema kuwa, Mji wa Mtwara ni mojawapo ya miji ambayo kwa sasa inanufaika na matumizi ya Gesi Asilia kwani mji huo umeunganishwa na miundombinu yenye jumla ya km 56.7 inayopeleka gesi kwa matumizi ya kuzalisha umeme, wateja wa majumbani, Taasisi na kiwanda cha Dangote.
No comments:
Post a Comment