Waziri wa Kilimo Mhe Prof.
Adolf Mkenda amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe Bilinith Mahenge, Uongozi
wa Wilaya za mkoa huo pamoja na wataalamu wote wa kilimo kwa kuitikia wito wa serikali
wa kutekeleza matakwa ya serikali katika kukabiliana na upungufu wa mafuta ya
kula.
Waziri Mkenda ametoa pongezi
hizo leo tarehe 25 Agosti 2021 katika Ofisi za Wizara ya Kilimo zilizopo katika
mtaa wa Tazara Jijini Dar es salaam wakati akizungumza na Mkuu huyo wa Mkoa wa Singida
akiwa ameambatana na wataalamu wa Kilimo.
Waziri Mkenda amesema kuwa
pamoja na mikoa yote kuitikia wito huo wa serikali katika kuongeza tija na
uzalishaji wa alizeti ili kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula kiasi kuagiza
mafuta nje ya nchi, mkoa huo wa Singida umeibuka na mkakati kabambe ili
kutekeleza maelekezo hayo ya serikali.
“Na wewe mkuu wa mkoa huna
makeke lakini mambo yako yanaonekana sana, na mimi nipende kukuahidi kuwa
serikali inaendelea na mkakati wa kuimarisha upatikanaji wa mbegu za alizeti
ili kuwa na mbegu bora na za kutosha“ Amekaririwa Waziri Mkenda
Waziri Mkenda ametoa wito kwa
wakulima wakubwa kuhakikisha kuwa wanaingia mkataba na Bodi ya Nafaka na Mazao
Mchanganyiko kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa mbegu pamoja na masoko.
Kadhalika amewasihi wakulima
wadogo kuhakikisha kuwa wanaingia mikataba na Taasisi za serikali kupitia Vyama
Vya Msingi Vya wakulima ili kurahisisha huduma hiyo ya upatikanaji wa mbegu
bora na masoko ya uhakika.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa
wa Singida Mhe Bilinith Mahenge amesema kuwa mkoa huo upo katika utayari mkubwa
kwa ajili ya kilimo cha alizeti kwani una ardhi ya kutosha na isiyokuwa na
migogoro kama ilivyo katika mikoa mingine nchini.
Amesema kuwa kwa kuanzia tayari
mkoa huo umetenga Hekari 596,000 kwa ajili ya kilimo cha alizeti huku akitoa wito
kwa serikali kuhakikisha mbegu zinapatiakana kwa wakati kwani jambo hilo likifanyika
kwa wakati itakuwa ni chachu kwa wakulima kuongeza ukubwa wa maeneo yao ya
kilimo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment