Wednesday, August 25, 2021

WATENDAJI ILEMELA WATAKIWA KUSIMAMIA SHERIA KWA HAKI

Watendaji wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela wametakiwa kusimamia sheria, kanuni na taratibu huku wakitenda haki kwa wananchi
Hayo yamebainishwa na mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Elias  Masalla wakati wa ziara yake ya awamu ya pili katika viwanja vya shule ya msingi Buswelu kata ya Buswelu ambapo amewataka watendaji wa wilaya hiyo kuhakikisha wanasimamia shughuli za ukusanyaji wa mapato, usafi na mazingira, ulinzi na usalama pamoja na utekelezaji wa shughuli nyengine zote za maendeleo kwa kushirikisha wananchi na kuwatendea haki katika utekelezaji wake

‘… Watendaji mnalojukumu la kusimamia sheria katika maeneo yetu, Lakini kwa kutenda haki asionewe mtu …’ Alisema

Aidha Mhe Masalla amewataka wananchi hao kumshukuru Rais Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kutenga na kutoa fedha kwaajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na itakayoanza kutekelezwa wilayani humo ikiwemo miradi ya ujenzi wa barabara ya Mbogamboga Buswelu-Nyamadoke Nyamhongolo, mradi wa ujenzi wa tanki la maji Buswelu, miundombinu ya elimu na afya huku akiwahakikishia upatikanaji wa chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 katika vituo vya afya vilivyochaguliwa katika wilaya hiyo na kuwaomba kujitokeza kwa hiari.

Kwa upande wake msajili wa mamlaka ya vitambulisho  vya taifa (NIDA) wilayani humo Bwana Adili Moshi amefafanua kuwa mpaka sasa wananchi 7620 wamekwisha tengenezewa vitambulisho na wale wenye uhitaji wa dharula wanaweza kufika ofisi za mamlaka hiyo kwaajili ya kupata msaada huku akiwaomba wananchi hao kufika katika ofisi ya kata yao kwaajili ya kuvichukua

Nae Bwana Gavidas Mlyuka kutoka wakala wa barabara za mijini na vijijini TARULA ametaja miradi mbalimbali itakayotekelezwa ndani ya kata hiyo ikiwemo ukarabati wa barabara za baadhi ya mitaa na madaraja ya mtaa wa Kigala yanayochangia adha kubwa kwa wananchi wa mtaa huo hasa wakati wa masika kushindwa kuendelea na shughuli za kila siku za maendeleo

Mhe Hassan Elias Masalla anaendelea na ziara zake za kutembelea kata 9 zilizosalia kwa awamu ya pili kwaajili ya kusikiliza kero, maoni na changamoto zinazowakabili wananchi wa wilaya hiyo akiambatana na wataalamu wa manispaa ya Ilemela, kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo na wakuu wa taasisi nyengine za Serikali zinazopatikana ndani ya wilaya hiyo ikiwemo TANESCO, TARULA, NIDA, RITA, MWAUWASA.

No comments:

Post a Comment