Na.Faustine Gimu Galafoni.
Mkutano wa wasaidizi wa huduma za sheria hapa nchini ulioandaliwa na Wizara ya katiba na sheria umehitimishwa jijini Arusha huku wadau wakitoa ushauri kwa serikali namna ya kupitia sheria mbalimbali ikiwemo kuangalia upya uendeshaji wa mabaraza ya ardhi ngazi za kata na wilaya ili kuweza kuondoa mianya ya rushwa inayoweza kujitokeza.
Akizungumza na mtandao huu mara baada ya kuhitimishwa mkutano huo wa siku mbili Msaidizi wa huduma za kisheria Malaki Kusekwa kutoka Wilayani Bunda mkoani Mara amesema mabara ya ardhi hutegemea posho kutoka kwa mlalamikaji na mlalamikiwa jambo ambalo linaweza kuchochea rushwa. .
“Tuishukuru sana wizara ya katiba na sheria kwa kuandaa mkutano huu nyeti katika masuala ya kisheria,jambo ambalo nimesisitiza ni kuhusu mabaraza ya ardhi ngazi ya kata kutokuwa na fungu na yamekuwa yakitegemea posho kutoka kwa mlalamikaji ama mlalamikiwa ili yaweze kuendesha kesi hali hii huchochea vitendo vya rushwa mtu akiwa na pesa ndiye mwenye uwanda mpanda wa kushinda kesi hivyo ni vyema jambo hilo likaangaliwa na kupitiwa upya ili mabaraza haya yasitegemee posho kutoka kwa wenye kesi”amesema.
Wakili Abia Richard kutoka kituo cha
Msaada wa kisheria kwa wanawake [Women Legal Aid Centre-WLAC] amesema pamekuwepo na changamoto ya kesi
kukaa muda mrefu bila kuamuliwa chanzo kikiwa ni baadhi ya mawakili wasiokuwa
waaminifu ambapo huwa wananunuliwa na watu wenye uwezo ili kuweza kuwatesa watu wa hali ya chini.
“Unakuta mama masikini anazunguka na majalada zaidi ya miaka miwili au mitatu hili tumeweza kulizungumzia katika kikao chetu kwa kuwa serikali yetu ni sikivu kupitia wizara ya katiba na sheria inaweza kuyafanyia kazi kwanza kuipongeza sana kwa kuona umuhimu wa mchango wetu kwa mstakabali mzima wa taifa letu”amesema.
Meneja mwandamizi wa program ya Mfuko wa
Ruzuku masuala ya sheria Tanzania[LSF] Deogratias Bwire Wamesema hali hii
huchochea vitendo vya rushwa kwani mlalamikaji au mlalamikiwa anayetoa fedha
nyingi hupewa kipaumbele zaidi na
kushinda kesi ambapo pia wasaidizi hao wa kisheria wamesema pamekuwepo kwa
changamoto ya kesi kukaa muda mrefu mahakamani chanzo kikiwa ni mawakili
wasiokuwa waaminifu kununuliwa na watenda makosa ili kuhalalisha kushinda kesi.
“Wadau wameainisha changamoto ya
tofauti ya takwimu na changamoto ya uratibu hivyo ushauri umetolewa kwa wizara
mtambuka kukaa pamoja katika kufanikisha masuala mbalimbali ya uratibu”amesema.
Kupitia mkutano huo wasaidizi hao wa huduma
za kisheria wamesema umewasaidia kuwajengea uwezo pamoja na kuweza kupitia
maboresho ya sheria huku wakitumia fursa hiyo kuipongeza wizara ya katiba na
sheria kwa kuwa mstari wa mbele kuwajengea uwezo.
Akihitimisha mkutano huo Msajili wa watoa Huduma ya msaada
Kisheria Felister Mushi amesema mkutano huo utakuwa chachu ya kufanya
maboresho ya mfumo wa utoaji haki.
“Huu ni mwendelezo tumeyapokea ambayo tumeyapokea mwisho wake tuweze kufanya maboresho katika mfumo mzima wa toaji wa haki kwa usawa ,lakini pia suala la uelewa,matumizi ya wanasheria kwenye halmashauri hivyo masuala kama hayo tunaendelea kuyafanyia kazi’’amesema.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika Mkutano huo wa siku mbili ni pamoja na huduma ya Msaada wa kisheria kabla ya kutungwa Sheria ya Msaada wa kisheria Na.1 ya mwaka 2017 pamoja na maboresho ya huduma ya Msaada wa kisheria chini ya Sheria ya Msaada wa kisheria Na 1 ya mwaka 2017.
No comments:
Post a Comment