Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema uwezo wa viongozi na makada wa chama hicho unatokana na utayari, uthubutu na kuujua umma unataka nini, kwa wakati upi na namna ya kutimiza mahitaji husika kulingana na changamoto zinazowakabili wananchi.
Pia kimesema chama cha siasa ambacho hakiwezi kuheshimu matakwa ya wanachama, wananchi na Taifa hutanguliza maslahi binafsi ya viongozi kuliko maslahi mapana ya umma kama wafanyavyo upinzani na hapo ndipo penye tofauti kati yao na chama tawala.
Hayo yamesemwa jana na katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka alipoulizwa iwapo CCM ina utofauti na upinzani alisema kuna utofauti kati ya viongozi wake na upinzani vivyo hivyo katika ubora wa muundo na sera CCM huwezi kukifananisha na chama chochote nchini.
Shaka alisema kwanza vyama upinzani hivyo ukiacha kuwa ni vichanga, havijawa na uzoefu wa kutosha, viongozi wake wamepatikana nje ya mifumo yenye kuaminika kwa jamii ikiwemo kutokimbazana na mahitaji ya wakati.
Alisema mfano chadema iwapo kingelikuwa kinafanya tathmini au tafiti za kisiasa toka kwa wanachama wake na makundi mengine ndani ya umma kutaka kufahamu ajenda ipi ni kipaumbele kwa wakati huu kati ya uchuni na katiba mpya, basi takwimu zingewaonesha kipaumbele namba moja ni uchumi.
Katika hili tunawakumbusha wakafanye rejea kwenye utafiti wa TWAWEZA sauti za wananchi ambao ulionesha vipaumbele vya wananchi na katika hivyo katiba haikuwepo, wananchi walitaja maji, afya, elimu, rushwa, miundombinu na uchumi.
Alisema kutokana na chama hicho (Chadema) kushindwa kufanya tafiti za msingi zenye kwenda sanjari na mahitaji ya wakati, ndiyo maana kila wakati kimekuwa kikijikuta kikishindana na nguvu za upepo kwa mujibu wa wakati ndio maana hakijui kama uchumi wa watu ni kipaumbele cha kwanza na vingine hufuata baadaye.
"Chama bora na makini hujikita katika tafiti za kitaalamu kila mara ili kuweza kufahamu mahitaji ya wananchi na Taifa pamoja na namna nzuri ya kuyakamilisha. Matakwa na mahitaji ya wakati yanapopishana na kuanza kuchomoza ukaidi wa viongozi ni dosari na kiashiria kuwa chama husika kimepoteza ushawishi wake na kipo hatarini kuingia makumbusho ya kisiasa. Nguvu ya ushawishi sio uwezo wa kupaza sauti bali ni uwezo wa kuyaishi mahitaji ya wakati kwa njia sahihi." Alisema shaka.
Alisema kila madhumuni, shabaha, sera na malengo yenu kadri mnapoitazama jamii hapo ndipo mnapotakiwa kusimama pamoja kama viongozi huku mkiwa mmejitayarisha, mnajiamini na kujitegemea kifikra katika msimamo mmoja wenye manufaa ya wengi.
Aidha katibu mwenezi huyo alisema viongozi wasiojiamini kamwe hawawezi kuendeleza malengo yao ya msingi. Maana hawana moyo wa uvumilivu na subira hivyo ni vigumu sana kumudu migogoro ndani ya vyama wanavyoviongoza. Vyama vya upinzani vina viongozi wa aina hii wasiojiamini ndio sababu migogoro haikomi na vinadumaa.
"Sifa ya CCM ni bidii, utayari, umoja wake madhubuti, subira na ustahimilivu. Hayupo anayeweza kutenda na kutekeleza mawazo au fikra zake bila kupatikana uamuzi na msimamo wa pamoja. Hivyo vikao ni muhimu sana kuliko uwezo binafsi wa mtu. Siku zote CCM huamua mambo yake kwa kutazama mahitaji ya wengi kupitia vikao" Alisema
Shaka alisema aina ya viongozi wenye kuelewa hayo na kuyasimamia huwezi kuwakuta kwenye vyama vingine badala yake huko jamii itakutana na wapigania madaraka, wapenda vyeo na utawala na wala hutawaona viongozi au wanasiasa makini.
"Yapo mataifa yenye katiba zinazoitwa katiba bora. Cha ajabu mataifa hayo yapo kwenye ukabila, milio ya risasi, mapigano na umwagaji damu wao kwa wao. Yote ni kwa sababu wanasiasa wanapambana kusaka vyeo na kutafuta urahisi wa kupata madaraka ya kiutawala. Tanzania imepata gharama kubwa kujenga misingi ya amani, umoja, mshikamano iliyonayo leo ikiwa imewekewa misingi thabiti kwenye katiba. Kwa sasa tushirikiane na tushikamane vizuri kujenga uchumi kwanza." Alisisitiza shaka
Mwisho
No comments:
Post a Comment