Monday, August 2, 2021

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO NA SUDANI YA KUSINI KUUZA UNGA NA MTAMA MWEUPE-WAZIRI MKENDA

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akikagua huduma za ununuzi wa nafaka mara baada ya kutembelea na kukagua kinu cha usagaji nafaka cha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), tarehe 2 Agosti 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akikagua akikagua hali ya uhifadhi wa unga unaozalishwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), tarehe 2 Agosti 2021 akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mjini Iringa.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) Dkt Anslem Moshi mara baada ya kukagua  hali ya uhifadhi wa unga unaozalishwa na Bodi hiyo, Leo tarehe 2 Agosti 2021 akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mjini Iringa.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) mkoa wa Iringa Karungi Titina mara baada ya kukagua utendaji kazi wa Bodi hiyo, Leo tarehe 2 Agosti 2021 akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja Mjini Iringa.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Iringa

Serikali imekamilisha mazungumzo na kampuni ya ubia ya Sudani ya Kusini kwa ajili ya kuuza unga pamoja na mtama mweupe.

Hiyo ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara nchini kwani wanatakiwa kuchangamkia fursa hiyo ambayo itakuwa sehemu ya muarobaini wa soko la nafaka kwa wakulima nchini.

Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 2 Agosti 2021 mjini Iringa mara baada ya kutembelea na kukagua kinu cha usagishaji nafaka cha Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).

Kuhusu kadhia ya uzalishaji duni wa mazao mbalimbali hususani nafaka Waziri Mkenda amesema kuwa serikali inaendela kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kuongeza tija kwenye mazao kadhalika kuongeza uzalishaji.

“Kuna uwezekano wa kuzalisha gunia 40 katika hekari moja hivyo ni lazima tuweke msisitizo kwenye kuongeza uzalishaji na tija” Amekaririwa Waziri Mkenda

Amesema kuwa pamoja na kuongeza tija na uzalishaji lakini ili kufikia hatua kubwa katika uzalishaji na tija hivyo ni lazima kuimarisha sekta ya mbegu na kuwa na upatikanaji wa mbegu bora nchini.

Kuhusu bei ya mahindi, Prof Mkenda amesema kuwa bei ya mahindi iliporomoka hivi karibuni ambapo aliagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) pamoja na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB)  kuingia sokoni ili kununua nafaka hususani mahindi jambo ambalo limeanza kuimarisha bei ya mahindi.

Katika ziara hiyo ya Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda kwenye mikoa ya Nyanda za juu kusini imejikita katika kugagua hali ya upatikanaji wa mbolea, ununuzi wa mahindi pamoja na kukagua skimu za umwagiliaji.

MWISHO

4 comments:

  1. Safi sana. Maisha ya mkulima lzima yainuke. Hongereni

    ReplyDelete
  2. Hongera Sana waziri tunaomba pia mipunga itoke nje maana wakulima wa mipunga tunahangaika Bei iko chini Sana

    ReplyDelete