Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt John Jingu amewaagiza maafisa ustawi wa jamii kutimiza majukumu yao kwa kufuata kanuni zilizowekwa ili kuepusha madhara mbalimbali yanayotokana na ukiukwaji wa sheria.
Akizungumza na Maafisa Ustawi pamoja na wadau mbalimbali mjini Morogoro, Dkt. Jingu amesema baadhi ya madhara ya kutotimiza wajibu ni pamoja na watoto kufanyiwa ukatili katika jamii zinazowazunguka.
“Kifungu namba 158 cha Katiba ya nchi yetu kinazungumzia juu ya wajibu wa wanajamii na watu wanaomiliki sehemu za starehe kutokuruhusu utoaji wa burudani kwa watoto nyakati za usiku. Bado wanajamii wanawatumia watoto kwenye utoaji wa burudani nyakati za usiku na hata wazazi kuwatuma watoto wao kwenye sehemu hizo kununua vitu kama sigara na Vilevi.” alisema Dkt Jingu.
Aliongeza kuwa Serikali pamoja na wadau wa masuala ya ustawi wa jamii imeona kuna haja wa kuweka kanuni na sheria zinazohusu maadili katika lugha rasmi na rahisi kwani kanuni zipo lakini pengine wanajamii hawazielewi.
Aliendelea kwa kusema kwamba kumekuwa na wimbi la watu mbalimbali wanaodhalilisha watoto kwa kutokufuata kanuni zilizowekwa.
“Baadhi ya wadau wanafanya baadhi ya mambo kwa nia nzuri lakini wanajikuta wanakosea. siku hizi kuna tabia ya kuwadhalilisha watoto waliofanyiwa ukatili kama kubakwa kwa kuwaweka kwenye mitandao bila kujali kuwa kile kitu kitakuwa na madhara ya kudumu kwa mtoto yule maana kuweka kitu kwenye mtandao ni kuipa nafasi dunia nzima kuona”
Dkt John Jingu alimalizia kwa kusema kuwa urahisishaji wa lugha inayotumika kwenye kanuni na sheria unaweza ukasaidia kupunguza makosa yanayojitokeza kwa wanajamii kushindwa kuzitasfiri vyema kanuni hizo.
No comments:
Post a Comment