Wednesday, August 11, 2021

DC MASALLA AWAHAKIKISHIA UPATIKANAJI WA CHANJO WANANCHI

Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla akizungumza na viongozi wa kata ya Kawekamo Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla akizungumza na wananchi wa kata ya Kawekamo wakati wa mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wananchi katika viwanja vya eneo la wazi Kawekamo’B’

MKuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla akikagua ujenzi wa miundombinu ya shule ya msingi Kilimani kata ya Kawekamo.

Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla amewahakikishiwa upatikanaji wa chanjo ya ugonjwa wa UVIKO-19 bila gharama yeyote wananchi wa wilaya hiyo na kuwaasa kujitokeza kwa hiari kwaajili ya kuchoma chanjo hiyo katika vituo vya afya vya Buzuruga, Karume na Kirumba.

Mhe Masalla amebainisha hayo wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Kawekamo wakati wa muendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi ambapo amewataka wananchi kupuuza propaganda hasi zinazoenezwa dhidi ya chanjo hiyo na kusisitiza kuwa Serikali ipo makini na hakuna kiongozi yeyote mwenye nia ovu ya kudhuru watu anaowaongoza

‘.. Mhe Rais anatupenda, anajua baadhi ya wananchi wake hawana uwezo wa kugharamia chanjo hii, ametuletea bure bila gharama yoyote, halazimishwi mtu kuchoma ila kwa hiari tunaweza kujitokeza kuchoma chanjo ..’ Alisema

Aidha Mkuu huyo wa wilaya mbali na kuwapongeza kwa namna wanavyojitoa katika shughuli za maendeleo akafafanua kuwa kwa wilaya ya Ilemela zaidi ya chanjo elfu tisa na mia sita zimepokelewa na kusambazwa katika vituo vya afya vilivyopangwa kwaajili ya zoezi hilo na kuongeza kuwa makundi maalum yamepewa kipaumbele katika uchomaji wa chanjo hiyo wakiwemo wazee wenye umri wa zaidi ya miaka hamsini, wataalam wa afya na askari.

Kwa upande wake mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndugu Shukran Kyando amewataka wananchi kuendelea kufuata ushauri unaotolewa na wataalam wa afya dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19, Pamoja na kuzingatia sheria za ardhi na mipango miji ikiwemo kutovamia maeneo wazi na Serikali haitawavumilia wananchi watakaovamia maeneo hayo na kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwavunjia nyumba zao

Bi Joyce George ni moja ya wananchi waliojitokeza katika kuwasilisha kero zao kwa mkuu huyo wa wilaya ambapo mbali na kumpongeza na kumshukuru kwa kuanzisha utaratibu huo wa kuwafata wananchi kwaajili ya kusikiliza kero zao amelalamikia ubovu wa baadhi ya barabara za kata hiyo na changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji kwa uhakika.

No comments:

Post a Comment