Nimepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa ya msiba wa Basil Pesambili Mramba.
Historia ya maisha, wasifu na haiba yake vilitosha kumfanya kuwa ni kiongozi wa kutegemewa na sisi sote hata baada ya kondoka kwenye nafasi rasmi za uongozi wa kisiasa. Tumempoteza kiongozi shupavu, mwenye busara, uvumilivu na uungwana mkubwa.
Mheshimiwa Mramba amekuwa mbunge wa Rombo kwa jumla ya miaka ishirini. Alitumia nafasi yake ya ubunge kuijenga na kuendeleza Wilaya ya Rombo. Sisi wana Rombo tutamkumbuka kwa mengi na hatutasahau kamwe mafanikio aliyotuletea.
Mheshimiwa Mramba aliwahi kuwa Waziri katika wizara mbalimbali, na atakumbukwa sana kwa utumishi uliotukuka. Kati ya mambo ambayo Mramba atakumbukwa sana ni juhudi zake za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini. Wengi tutakumbuka jinsi, akiwa Waziri wa Fedha, aliondoa kodi na tozo ambazo zilikuwa kero kwenye uchumi wetu.
Pamoja na madhila yaliyompata baada tu ya kuondoka kwenye nafasi ya ubunge, Mramba hakuwa na kinyongo na aliendelea kuwa mcheshi na kupigania maendeleo ya Rombo na Taifa hili kwa moyo mmoja. Mungu alimjalia moyo mkuu na wa ukarimu. Rombo na Taifa letu tumempoteza kiongozi mahiri. Mimi binafsi nimepoteza kiongozi niliyemheshimu sana na aliyenishauri sana kwenye mambo mengi.
Natoa pole nyingi kwa mjane wa marehemu Mramba, watoto, ndugu na jamaa wote kwa msiba huu.
Pamoja na huzuni, tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya Basil Pesambili Mramba. Tuadhimishe maisha yake na tunamwombea kwa Mungu ampe pumziko la amani, AMINA.
Prof. Adolf F. Mkenda.
MBUNGE
No comments:
Post a Comment