Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ameeleza kuwa serikali inaendelea na mkakati wa kuimarisha bei za mazao ya kilimo.
Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara ya Kilimo Jijini Dar es salaam ambapo amebainisha kuwa Serikali inapenda kuwaona wakulima wanapata faida kutokana na kilimo, ndiyo maana haijaweka kodi yoyote kwenye mbolea kama wengine wanavyozusha.
Amesema kuwa uzalishaji wa mazao una gharama kubwa japo bei za mazao kuna wakati zinakuwa hazieleweki.
“Bei ya mazao ya mahindi kwa sasa inazua taaruki kwenye baadhi ya mikoa, kwani yanauzwa kwa bei ndogo tofauti na gharama za uzalishaji alizotumia mkulima, hii inamkandamiza anaweza kushindwa kumudu gharama za pembejeo,” Amesema.
Kuhusu suala la mbolea, Waziri Mkenda amesema kuwa suala la mbolea limezua taaruki ambapo baadhi ya watu wamedai kuwa kupanda kwa bei ya pembejeo hiyo inachangiwa na kodi iliyowekwa na serikali.
“Hakuna kodi yoyote iliyowekwa kwenye mbolea kwa kuwa Serikali imelenga katika kuhakikisha inapatikana kwa bei nafuu ili kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea ambayo inawasaidia kuvuna mazao mengi,” Amesema Waziri Mkenda na kuongeza kuwa
“Tunaamini hatua hii itasaidia mbolea kuingia kwa wingi nchini hivyo wafanyabishara watakuwa na bei ya ushindani ambayo haimuumizi mkulima, pia tunachoangalia sisi mbolea inayoagizwa iwe na viwango vya ubora unaotakiwa,”
Amesema mfumo wa zabuni haujawasaidia kwa kuwa licha ya kuwa makampuni mengi yalikuwa yanajitokeza yanachakuliwa machache kisha bei inapangwa lakini siyo rafiki kwa wakulima.
“Japo hatuna uwezo wa kushusha bei kwenye soko la dunia lakini tunahitaji kuona wafanyabiashara wanasaidia kuwezesha mbolea kupatikana kwa wingi, Serikali inafanya juhudi kila inavyoweza ikiwamo hata kupunguza gharama za kulipia maghala ya kuhifadhia nafaka,” Amekaririwa Mhe Waziri
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) Dkt Anselm Moshi amewaeleza waandishi wa habari kuwa Bodi hiyo inanunua mahindi kwa bei nzuri ukilinganisha na bei iliyopo sokoni.
Dkt Moshi ameeleza kuwa ununuzi wa mahindi ni kati ya shilingi 250 hadi 480 ambapo bei inatofautiana kwenye mikoa husika.
“Wilaya ya Nkasi mahindi yanauzwa 250 hadi 270 kwa kilo moja, kanda ya kaskazini yanauzwa kwa bei ya shilingi 450 hadi 485 kwa kilo, hivyo bodi imeshatuma jumla ya shilingi bilioni 7.47 ya kununua jumla ya tani 14,948 kwa wastani wa shillingi 500 kwa kilo,” Amesema Dkt Moshi
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Ndg Militon Lupa amesema kuwa wakala unatarajia kununua takribani tani 165,000 za aina tatu za nafaka kwa msimu wa mwaka 2021/2022 kutoka kwenye mikoa yenye uzalishaji mkubwa kati ya hizo mahindi yatanunuliwa tani 150,000.
Lupa amesema kuwa katika kipindi kirefu NFRA imekuwa ikinunua mahindi pekee ambapo hivi sasa imeanza kununua nafaka aina ya mahindi, Mtama na mpunga
MWISHO
No comments:
Post a Comment