Thursday, July 15, 2021

SERIKALI YAWAPONGEZA WANANCHI WA BUHIGWE KIGOMA KUJITOA KATIKA MAENDELEO

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwasili katika Kijiji cha Kibuye, Kata ya Bukuba, Wilayani Buhigwe, Mkoa wa Kigoma alipokwenda kushiriki na wananchi katika ujenzi wa Zahanati ya Kata hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina akipokea shilingi 500,000/= kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis ikiwa ni mchango wake kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kibuye Wilayani Buhigwe.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akishiriki katika shughuli za Ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kibuye, Wilayani Buhigwe Mkoa wa Kigoma alipofanya ziara Wilayani humo.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Bukuba wakishuhudia ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Kibuye walipotembelewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis kwa ajili ya kuona shughuli za maendeleo zinazofanywa na wananchi.

Kiongozi wa Kikundi cha wanawake wa wa Kikundi cha Nyamunyinya, Monica Tuza akipokea mchango kutoka kwa Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis kwa ajili ya kuchangia shughuli za kikundi hicho ikiwa ni pamoja kukamua mafuta ya mawese.

Na Mwandishi Wetu, Buhigwe Kigoma

Serikali imewapongeza wakazi wa Kata ya Bukuba Wilayani Buhigwe mkoani Kigoma kwa juhudi zao za kuchangia mipango ya maendeleo ya Jamii ili kujikwamua na wimbi la umasikini.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mwanaidi Ali Khamis alipofanya ziara wilayani humo na kuwakuta wananchi wakiendelea na kazi ya kujenga Zahanati kwa kujitolea na kuchangia nguvu zao ambapo wamechangia kiasi cha sh. milioni 14 kati ya sh. milioni 65 zinazohitajika kukamilisha jengo hilo.

Naibu Waziri Mwanaidi amesema kuwa Serikali inafarijika kuona wananchi wakijitolea kujiletea maendeleo na kuongeza kuwa Serikali ya awamu ya sita itahakikisha inaboresha huduma kwa wananchi kama ilivyobainishwa katika vipaumbele vyake.

Akiwa katika Zahanati hiyo, Naibu Waziri Mwanaidi ameshiriki shughuli za ujenzi wa zahanati hiyo kwa kuchanganya mchanga na baadaye kutoa mchango wake wa shilingi laki tano kwa ajili ya maendeleo ya ujenzi huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu kwenye sekta mbalimbali hasa upande wa Afya hali inayosaidia wananchi wanakuwa na Afya njema ya kufanya kazi na kujiletea maendeleo yao.

Amesema kuwa Wananchi wa Wilaya hiyo wanaona fahari kutembelewa na kuungwa mkono na viongozi wa kitaifa katika juhudi zao za kujiletea maendeleo na utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Akiwa ziarani katika Kata hiyo ya Bukuba, Naibu Waziri Mwanaidi amepokea baadhi ya changamoto za eneo hilo ikiwa ni pamoja na idadi ndogo ya watumishi katika kada mbalimbali zikiwemo za Afya, Elimu na Ustawi na Maendeleo ya Jamii.

Aidha, Mhe. Mwanaidi ametembelea kikundi cha wanawake wanaojishughulisha na ukamuaji wa mafuta ya mawese na kuwahakikishia kwamba Serikali inaendelea kuwawezesha wanawake vijana na wenye ulemavu ili wajiunge katika vikundi na kukopeshwa mikopo isiyo na riba.

Amesema makundi hayo katika jamii hayana sababu ya kuwa na wasiwasi kwa kuwa Serikali imewaandalia mazingira ya kukopa kutokana na asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Kwa upande wao wananchi wa Wilaya ya Buhigwe wameishukuru Serikali kwa kuwaunga mkono katika jitihada zao za kujiletea maendeleo kwa kuwasaidia rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya kumalizia miradi mbalimbali Wilayani humo.

No comments:

Post a Comment