Waziri wa Kilimo Profesa Adolph Mkenda
(katikati) akikata utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa Kampuni ya Pass Leasing
itakayokuwa inajishughulisha na kukopesha wakulima, wavuvi na wafugaji zana za
kilimo bila dhamana kwa riba nafuu katika hafla iliyofanyika wakati wa Wiki ya
Pass Trust kwenye viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma Julai 24,2021.
Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Athony Mtaka na kulia kwake ni
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Pass Trust, Dkt. Tausi Kida. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Profesa Adolph Mkenda
(kulia), akimkabidhi ufunguo Anthony Maganga ikiwa ni ishara ya kumkabidhi
trekta aina ya New Holland yenye thamani ya sh. nil. 54 ikiwa ni mkopo
uliotolewa na Kampuni ya Pass Leasing. Anayeshuhudia katikati ni Mwenyekiti wa
Bodi ya Wadhamini ya Pass Trust, Dkt. Tausi Kida.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka (kulia),
akimkabidhi Namba ya usajili (Plate No) Anthony Maganga ikiwa ni ishara
ya kumkabidhi trekta aina ya New Holland yenye thamani ya sh. nil. 54 mkopo
uliotolewa na Kampuni ya Pass Leasing.
Waziri wa Kilimo Profesa Adolph Mkenda,
akimkabidhi ufunguo Lillian Maricky wa Kampuni ya Magic LN Suppliers ya
Chalinze, mkoani Pwani ikiwa ni ishara ya kumkabidhi mitambo ya kuvuna
mpunga yenye thamani ya sh. mil.79 mkopo uliotolewa na Kampuni ya Pass
Leasing. Anayeshuhudia katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Pass
Trust, Dkt. Tausi Kida.
Waziri wa Kilimo. Profesa Adolph Mkenda
(kulia), akimkabidhi ufunguo Gebe Millinga ikiwa ni ishara ya
kumkabidhi trekta aina ya John Deere pamoja na majembe yake lenye thamani ya
sh. mil. 71.4 mkopo uliotolewa na Kampuni ya Pass Leasing. Anayeshuhudia
katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Pass Trust, Dkt. Tausi Kida.
Gebe amepokea trewkta hilo kwa niaba ya kaka yake Mwanzo Millinga
anayefanya kazi ya kilimo mkoani Ruvuma.
Waziri wa Kilimo Profesa Adolph Mkenda akimkabidhi ufunguo Dickson Tesha ikiwa ni ishara ya kumkabidhi trekta aina ya New Holland lenye thamani ya sh. mil. 46 mkopo uliotolewa na Kampuni ya Pass Leasing. Tesha amepokea trekta hilo kwa niaba ya Japhet Ndebesi wa Chamwino, mkoani Dodoma.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali kwa kushirikiana na taasisi za fedha imejipanga kuagiza
mbegu bora na kuzigawa kwa wamiliki wa viwanda vya mafuta nchini ili waweze
kuingia mikataba na wakulima wakubwa, au vyama vya Ushirika ambavyo vitaingia mikataba
na wakulima ili kuwapatia mbegu hizo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji na tija
katika mazao ya kilimo.
Waziri wa Kilimo Mhe. Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 24
Julai 2021 katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma wakati
akizindua shughuli za Kampuni ya PASS Leasing ambayo ni kampuni tanzu ya
PASS Trust, iliyosajiliwa na benki kuu, kutoa huduma za kukopesha mikopo ya
zana za kilimo bila dhamana.
Waziri Mkenda amesema kuwa changamoto inayoikabili sekta ya
kilimo ni uchache wa uzalishaji mbegu nchini, Uwezeshaji wa Maafisa Ugani
pamoja na Zana za Kilimo, hivyo ili kukabiliana na changamoto hizo tayari
serikali imekuja na muarobaini.
Mafuta ya alizeti ni mazuri kuliko mengine hivyo katika
kuimarisha afya za watanzania, mkakati huo wa kuongeza uzalishaji na tija
katika mazao ya mafuta hususani zao la alizeti itaimarishwa ambapo tayari mikoa
mitatu ya Simiyu, Singida na Dodoma imewekwa kama mikoa ya mfano katika
uzalishaji.
Akizungumzia kuhusu Maadhimisho hayo, Waziri Mkenda amesema kuwa
wiki ya kilimo kwa PASS Trust ambayo inafanyika jijini Dodoma, chini ya kauli
mbiu “Pamoja tuwezeshe upatikanaji wa fedha kwa kilimo endelevu, kwa
ushirikiano na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe Antony Mtaka imeandaliwa
wakati muafaka ambapo serikali inatilia mkazo kampeni zinazolenga kuinua kilimo
cha mazao ya kimkakati nchini.
Katika hafla hiyo, Waziri Mkenda amezindua Kampuni ya Pass
Leasing ya kukopesha wakulima zana za Kilimo bila dhamana na kwa riba nafuu
pamoja na kukabidhi zana za kilimo za kisisa kwa wateja wanne wa kwanza ambazo
ni matrekta matatu na mtambo wa kuvunia mpunga.
Waliokabidhiwa ni; Kampuni ya Magic LN Suppliers ya Chalinze
mkoani Pwani ambayo imekopeshwa mtambo wa kuvunia mpunga wenye thamani ya sh.
Mil. 79, Anthony Maganga wa Igunga Tabora aliyepata Trekta aina ya New Holland
lenye thamani ya sh. Mil. 54.
Wengine ni Japhet Ndebezi wa Chamwino mkoani Dodoma
aliyekopeshwa Trekta lenye thamani ya sh. Mil. 46 na Mwandishi wa Habari Mwanzo
Millinga wa Ruvuma ambaye amepata Trekta aina ya John Deere pamoja na majembe
yake lenye thamani ya sh. Mil. 71.4.
Makabidhiano hayo yamefanyika mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka na viongozi wa Taasisi Pass Trust pamoja na wananchi waliohudhuria Wiki ya Pass Trust kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.
Mikopo inayotolewa na Kampuni ya Pass Leasing kwa upande wa kilimo ni; zana za kuwezesha uzalishaji wa kilimo cha mazao, usindikaji, uhifadhi wa mazao na usafirishaji.
Kwa upande wa uvuvi ni; vifaa uvuvi na mashine zote zitumikazo kuongeza tija
katika sekta ya uvuvi. Ufugaji nyuki ni; Vifaa mbalimbali vya kuongeza
tija na thamani katika sekta ya nyuki na mazao yatokayo na na
nyuki.
Ufugaji ni; Vifaa na mashine za kuongeza tija katika sekta ya
ufugaji na kwa upande wa misitu ni vifaa na mashine zitumikazo kwenye misitu na
viwanda vya mbao.
MWISHO
No comments:
Post a Comment