Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (wa pili kushoto) akifungua pazia kuashiria uzinduzi rasmi wa Nyumba 24 za Makazi katika eneo la Inyonga wilayani Mlele mkoa wa Katavi tarehe 20 Julai 2021.
Na Munir Shemweta, KATAVI
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limewekeza kiasi cha shilingi bilioni 7.3 katika Mkoa wa Katavi baada ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi katika mkoa huo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa nyumba za makazi Inyonga uliofanywa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula katika wilaya ya Mlele mkoani Katavi tarehe 20 Julai 2021, Meneja wa Shirika la Nyumba mikoa ya Rukwa na Katavi Injinia Patrick Kamendu alisema, miradi iliyotekelezwa ni pamoja na ile nyumba za makazi katika maeneo ya Ilembo, Inyonga, Kakuni na jengo la Kitega Uchumi la Mpanda Plaza.
Hata hivyo, aliongeza kuwa, pamoja na uwekezaji huo, NHC imejenga kama Mkandarasi Jengo la Ofisi la Wakala wa Misitu Tanzania(TFS) lililogharimu shilingi milioni 263 ambalo alilieleza kuwa limekamilika na lishakabidhiwa kwa wahusika.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alilipongeza Shirika la Nyumba la Taifa kwa kufanikisha kutekeleza miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi kwenye mkoa huo wa Katavi kwa ufanisi.
Alilitaka shirika la Nyumba la Taifa kuongeza kasi ya ujenzi wa miradi katika eneo la Inyonga palipojengwa nyumba za makazi ili kukidhi kiu ya wananchi wanaohitaji nyumba za kuishi.
“Nawasihi muongeze kasi ya ujenzi wa nyumba za makazi katika maeneo haya kwani uhitaji ni mkubwa ili mlele paweze kuvitia na watu waendelee kwenda kuishi” alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Meneja wa NHC mikoa ya Rukwa na Katavi, eneo la Inyonga palipojengwa nyumba za makazi ni maeneo ya viwanja 70 vilivyonunuliwa na shirika kutoka kwenye halmashauri ya wilaya ya Mlele. Pia, kuna viwanja vilivyobaki alivyovieleza kuwa vitaendelezwa hapo baadaye.
Akielezea zaidi mradi wa Inyonga, Meneja huyo wa NHC alibainisha kuwa, mradi huo umetekelezwa katika halmashauri ya wilaya ya Mlele na kuwekewa jiwe la Msingi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Ndugu Abdulrahaman Kinana.
Kwa mujibu wa Injinia Kamendu, mradi huo una jumla ya nyumba Ishirini na nne(24) za makazi (semi detached) na ulianza kutekelezwa mwezi Juni 2014 kwa kutumia vyanzo vya ndani vya mapato ya Shirika.
Hadi kukamilika, mradi wa nyumba wa Inyonga umegharamu shilingi 991,482,480.00 ambazo ni fedha za mapato ya ndani ya shirika ambazo zinazotumika kuongeza mapato ya mikoa midogo na kuhakikisha kwamba huduma za shirika zinafika katika mikoa yote nchini.
No comments:
Post a Comment