KIONGOZI Mkuu wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala amewataka viongozi wa kisiasa na kidini kuacha kutumia ushawishi walio nao katika jamii kuipinga chanjo ya virusi vya corona.
“Nampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa hekima yake ya kuruhusu chanjo ije nchini kwa ajili ya ustawi wa afya za wananchi wetu wa Tanzania;
Wito huo ameutoa muda mfupi baada ya maombi ya kuliombea Taifa ambayo alikuwa anayafanya maalum Yespa, Kihond mjini Morogoro ili Mungu aweze kuiponya Tanzania na watu wake huku akisisitiza kuwa, licha ya maombi pia ni jukumu la kila mmoja kuzingatia miongozo na kanuni zinazotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya ili kukabiliana na Corona.
“Ushauri wangu kwa viongozi wa kijamii hasa viongozi wa dini tusitumie ushawishi tulio nao miongoni mwa jamii yetu kupinga suala la chanjo, hilo ni jambo ambalo linaweza kuligawa Taifa na kulifanya lisitawalike na jambo ambalo si nzuri kwa kuwa linawazoeza watu kupingana na maamuzi ya mamlaka za nchi.
“Tabia hii ya viongozi wa dini kuipinga Serikali hadharani wakati tunayo fursa ya kuishauri Serikali bila vipaza sauti kwa hakika inatengeneza watu wenye kiburi wasiotii viongozi wa nchi na kutokutii mamlaka maandiko yanasema ni uasi na huko ni kugombana na Mungu,”alifafanua Nabii Dkt.Joshua.
Pia aliwaomba wananchi wasiogope juu ya chanjo, “Serikali yetu ipo makini sana na inaongozwa na Mungu, kamwe haiwezi kuwaangamiza watu wake. Mwisho namuomba Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aendelee kuwaa hodari na moyo wa ushujaa, asiyumbe anapoyumbishwa sisi wananchi na kanisa tunamuombea sana na tupo pamoja na serikali yake.
“Mimi binafsi ninamwahidi kuwa nitazunguka nchi nzima kwa gharama zangu kuisaidia Serikali kutoa elimu kwa wananchi ili waokoe afya zao dhidi ya Corona kwa njia ya chanjo,”alisema Nabii Dkt.Joshua.
Wito huo ameutoa ikiwa leo Julai 28, 2021 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiongozana na viongozi mbalimbali waandamizi wa Serikali wamezindua rasmi chanjo ya corona nchini.
Uzinduzi huo umefanyika Ikulu jijini Dar es Salaam ambapo Rais Samia Suluhu Hassan amesema chanjo hiyo ni salama na asingekuwa tayari kuhatarisha maisha yake kwa kuchanjwa chanjo ya Corona kama ingekuwa si salama.
Hatua hiyo inakuja baada ya wiki iliyopita Tanzania kupokea zaidi ya dozi milioni 1.05 za chanjo aina ya Johnson & Johnson zilizotolewa na Marekani kupitia mpango wa upatikanaji wa chanjo wa Covax.
Katika mpango huo, wapo baadhi ya watu wanaopingana na harakati hizo wakieleza chanjo hizo sio salama na wapo wanaounga mkono, lakini kiongozi huyo mkuu wa nchi amewaondoa hofu wananchi kuhusiana na hilo.
Rais Samia alisema yeye ni mama wa watoto wanne, ni bibi wa wajukuu kadhaa wanaompenda sana na yeye kuwapenda, ni mke pia lakini mbali ya yote ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi wa nchi hii.
“Nategemewa kama mama, kama bibi, kama Rais, kama Amiri Jeshi Mkuu, nisingejitoa mwenyewe nikajipeleka kwenye kifo, nikajipeleka kwenye hatari nikijua kwamba nina majukumu yote haya yananitegemea .
“Lakini nimetoka kuonyesha umma wanaonifuata nyuma nikijua kama Rais ni mchungaji na nina watu wengi nyuma nawachunga na wananitazama mimi hivyo nisingetoka kujihatarisha,”amesema Rais Samia.
Rais amebainisha kuwa amekubali kwa hiari yake kuchanja akijua kwamba ndani ya mwili wake ana chanjo kadhaa ambazo ameishi nazo kwa miaka 61 sasa kwani tangu amezaliwa kuna chanjo mbalimbali wamekuwa wakichanjwa, mbali na zingine wanazochanjwa njiani wakiwa wanasafiri ikiwemo ya homa ya manjano.
Hivyo kwake haoni hatari iliyoko na baada ya wanasayansi kujirishisha hivyo yupo tayari kuchanja na kuwa kuwaomba Watanzania wapuuze yote wanayoyasikia kuhusiana na chanjo hiyo.
“Kwa wale ambao koo zao hazijaguswa, hawajapata madhara ya maradhi haya wanaweza kusema wanavyotaka. Lakini nenda leo Moshi, nenda Arusha ,nenda Kagera, hata Dar es Salaam uonane na zile koo ambazo zimeshaguswa na haya maradhi wana maneno ya kukuambia na kama wangeweza leo wote wangekuwa hapa kutaka kuchanja kuepukana na ile hasara walioipata,”alisema.
No comments:
Post a Comment