Waziri wa nishati Medard Kalemani amemtaka mkandarasi anayesambaza umeme kampuni ya Namis Cooparate Limited Kata ya Shibula wilayani Ilemela mkoani Mwanza kuhakikisha anakamilisha kwa wakati ili wananchi hao waanze kuutumia kwa shughuli za maendeleo.
Aidha amesisitiza gharama ya kuunganishiwa umeme wa Pari Urban kuwa ni 27,000 na asiwepo mwananchi yoyote ambaye atambiwa kulipia nguzo kwani nguzo hutolewa bure.
Mhe. Kalemani alisema hayo Julai 9, 2021 Mtaa wa Ilalila kata ya Shibula Mkoani humo wakati wakati akizungumza na wananchi, mkandarasi a viongozi mbalimbali kwenye hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika MRADI WA KUSAMBAZA UMEME AWAMU YA PILI KATIKA MAENEO YA PEMBEZONI MWA MJI NA MAJIJI.
“Hii ni kampuni mara zote imekuwa ikifanya vizuri na ina kumbukumbu nzuri ndo maana Mbunge tumekuletea hapa, tuna imani itapeleka umeme katika maeneo yote 38 ndani ya miezi 12 na ikibidi waokoe miezi miwili na hakutakuwa na muda nyongeza, na hata kama mnafanya vizuri hatutasita kuwashughulikia kama mtaenda kinyume na makubaliano” alisema
Ameongeza kuwa iko tabia ya kusema nje ya scope hapa ni wateja 970 au 1000 lakini wako wengine wapo ndani amemtaka mkandarasi kushirikiana na Tanesco kama wako nje ya scope Tanesco watandaze umeme kama wako ndani Mkandarasi atandaze umeme, na kusisitiza kama maelekezo ya serikali hakuna mwananchi kuuziwa nguzo.
Mbali na hilo alimtaka mkandarasi huyo kuhakikisha anafaya kazi usiku na mchana na vibarua watoke katika katika maeneo hayo sambamba na kuhakikisha baada ya malipo ndani ya siku 14 mwananchi anaunganishiwa umeme.
“Tuna amini kuwa miradi hii inapokuja mbali na kuleta faida kwa wananchi, pia hutoa fursa za ajira kwa wananchi waliopo ndani ya mradi, hivyo naelekeza vibarua watoke hapa hapa, sio kuwatoa watu Kagera, Shinyanga na kwingineko kuja kufanya kazi hii, hapana vibarua watoke hapa hapa na hii itarahisisha kazi na itaenda kwa kasi” aliongeza
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt Angelina Mabula ambaye ni Naibu waziri wa Ardhi, Nyumba Maendeleo na Makazi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi baada ya maombi ya muda mrefu kufuatia kutokuwa na vigezo vya kuunganishiwa umeme wa REA ambao ulihusu vijiji na kuja na mpango wa PERI URBAN wa usambazaji wa umeme pembezoni mwa Miji na Majiji.
“Wananchi wa Ilemela hatuna budi kumshukuru Mhe. Rais kwa sababu ya hali halisi ambayo serikali ya awamu ya sita imeendeleza kile ambacho tulikuwa tunakitamani” alisema Mhe. Mabula
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Hassan Masala alimshukuru Mhe. Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya hususani katika kuwaletea wananchi maendeleo, akitoa shukrani pia kwa Mbunge wa Jimbo hilo kwa kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.
Akitoa taarifa ya mradi huo Meneja wa REA kanda ya ziwa ERNEST MAKALE alisema Peri Urban ni mradi unaotelezwa ukilenga maeneo ya Miji na Majiji ambayo hayakufikiwa na huduma ya umeme na hapa nchini unatekelezwa katika mkoa wa Dodoma, Arusha na kwa sasa hapa Mwanza ambapo unatekelezwa katika mitaa 59 kwa gharama ya shilingi bilioni 9.94 na kwa Ilemela mitaa 38 itasambaziwa umeme ambapo kiasi cha shilingi bilioni 6 zitatumika.
Mradi wa Peri Urban wa usambazaji wa umeme umelenga kufikisha huduma ya umeme katika maeneo yote yaliyokuwa yamesalia kufikiwa na nishati hiyo na kupitia mradi huo umeme utaunganishwa kwa shilingi 27,000.
No comments:
Post a Comment