Chama Cha Mapinduzi kimesema kwa hali inavyokwenda nchini kunataka kujengeka tabia ya kuonekana kuwa dawa na maji safi kwa wananchi ni suala la anasa wakati ni mahitaji muhimu kwa uhai wa maisha na uchumi.
Kimesema changamoto za upungufu mkubwa wa dawa, maji safi na salama pamoja na wawekezaji kucheleweshewa huduma za msingi za wao kuanza uzalishaji zimebainika jambo ambalo CCM haiwezi kuyavumilia.
Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo ameyasema hayo wakati wa majumuisho ya ziara yake na sekretariet mkoani Songwe katika ukumbi wa Mkonongo mkoani hapa.
Amefahanisha kuwa wananchi wanalipa kodi na wanachangia huduma hizo haiwezekani waliopewa dhamana wasiwasikilize na kufanya bidii ya kutatua kero walizo nazo.
"Kote tulikopita kilio ni dawa na maji safi, naomba niwahakikishie ndani ya wiki !moja baada ya kurejea Dodoma nitaziita wizara zote zinazohusika kutueleza hili limekaaje maana serikali inatenga mabilioni ya fedha na kila wakati kauli za tunazo dawa za kutosha zinatolewa wakati haziakisi uhalisia kwenye maeneo ya huduma kwa wananchi. Tunataka kujua tatizo ni nini, ili kutatua changamoto hii. Vivyo hivyo kwenye maji safi" alisema Chongolo
Chongolo amewataka wataalam wa halmashauri zote nchini kuhakikisha pale wanapoibua miradi ya kimkakati yenye kulenga kusisimua uchumi na kuongeza mapato kwenye maeneo yao wahakikishe inazingatia mahitaji na matakwa halisi ya watumiaji wa makundi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi hususani wananchi wa kipato cha chini na kati.
"Unapenda kubaki au kuendelea na cheo au dhamana uliyoaminiwa timiza wajibu kwa kuhakikisha wananchi wanaona fahari ya wewe kuwepo katika nafasi uliyopo vinginevyo hatutakubali kukuona hapo wakati unatugombanisha nao, hii ndio kazi ya CCM." Alisema Chongolo
Hata hivyo kizungumza kwa kutoa mfano Chongolo amesema haiwezekani unajenga mradi wa soko halafu jengo lenyewe la ghorofa unataka mama mbogamboga akauzie ghorofa ya kwanza, halafu mradi wa aina hiyo hauna eneo la bodaboda, bajaji, machinga na mama/baba lishe kufanya shughuli zao lazima utakuwa mradi kero.
"Hakuna raia wa daraja teule, sote tuna hadhi sawa. Miradi hii izingatie mahitaji na mazingira halisia ya watumiaji yakiwemo makubwa mbalimbali ya kiuchumi yanayoweza kunufaika nao ili kuimarisha mnyororo huo wa uchumi vinginevyo serikali itawekeza fedha kwenye miradi isiyoleta matokeo yaliyotarajiwa." Alisema Chongolo
Katibu Mkuu wa CCM na Sekretarieti yake wataendelea na ziara yao mkoani Mbeya kuanzia tarehe 11 Julai, 2021.
No comments:
Post a Comment