Friday, June 18, 2021

WAZIRI MKENDA AWEKA BAYANA FURSA ZA UWEKEZAJI MBELE YA BALOZI WA VIETNAM MHE NGUYEN NAM TIEN

Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akimkabidhi zawadi ya korosho Mgeni wake-Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Mhe Nguyen Nam Tien mara baada ya kufanya mazungumzo Jijini Dodoma, Tarehe 17 Juni 2021. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akimsikiliza kwa makini Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Mhe Nguyen Nam Tien wakati akisisitiza jambo kuhusu uwekezaji nchini Tanzania  mara baada ya kufanya mazungumzo Jijini Dodoma, Tarehe 17 Juni 2021.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akianisha fursa za Uwekezaji kwenye sekta ya kilimo zilizopo nchini Tanzania mbele ya mgeni wake Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Mhe Nguyen Nam Tien mara baada ya kufanya mazungumzo Jijini Dodoma, Tarehe 17 Juni 2021.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda na mgeni wake Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Mhe Nguyen Nam Tien wakitazama fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania wakati wakifanya mazungumzo Jijini Dodoma, Tarehe 17 Juni 2021.
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Mhe Nguyen Nam Tien mara baada ya kukamilika kwa mazungumzo yao Jijini Dodoma, Tarehe 17 Juni 2021.

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma


Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda jana tarehe 17 Juni 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Mhe Nguyen Nam Tien ambapo ameainisha fursa za Uwekezaji zilizopo nchini Tanzania katika sekta ya kilimo ambazo Vietnam inaweza kuwekeza.


Waziri Mkenda ameanisha maeneo ya kipaumbele ambayo nchi hiyo inaweza kuwekeza hapa nchini Tanzania ambayo ni pamoja na Uzalishaji wa mbegu (Seed Multiplication) zenye tija (Highly Productive Seeds), Uwekezaji katika kuzalisha mbolea za viwandani, Utafiti katika uzalishaji wa mbegu za mazao; Kununua mazao kutoka Tanzania kama tumbaku, korosho na kahawa aina ya arabika; na Mazao ya kimkakati ili kupunguza uagizaji wa bidhaa na mazao hayo kutoka nje kama ngano, shayiri na alizeti.


Maeneo mengine yaliyoanishwa na Waziri wa Kilimo Prof Mkenda kuhusu uwekezaji ni pamoja na kuwawezesha Maafisa ugani wa kilimo kwa sasa maafisa ugani hawafanyi kazi ipasavyo kwa kuwa hawana vitendea kazi; Kuanziasha mashamaba darasa- Farmers Field School ili kuwafundisha wakulima ujuzi mbalimbali kuhusiana na kilimo; na Kujenga miundombinu ya umwagiliji ili kuongeza uzalishaji.


Mengine ni Kupata mikopo ya kilimo (Agri- financing) Waziri Mkenda amesema kuwa Wizara inaandaa mkutano na wenye mabenki ili kujadili na kuona namna ya kukopesha sekta ya kilimo; Kuthibiti nzige wekundu (Control of Redlocust) Tanzania inajitahidi kuwekeza fedha kwa ajili ya kununua ndege ya Wizara kwa ajili ya kukabiliana na nzige na wadudu wengine waharibifu wa mazao ya wakulima; na Kuwajengea uwezo wataalam wa kilimo (Exchange Programmes).


Katika mazungumzo hayo Balozi wa Vietnam nchini Tanzania, Mhe Nguyen Nam Tien ambaye aliongozana na Bw. Le Minh Tuan Naibu Mkuu wa masuala ya Mahusiano na Bi. Amina Husein Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alimuhakikishia Waziri Mkenda kuwa wawekezaji wengi wa nchini Vietnam wangependa kuwekeza Tanzania kutokana na utulivuli uliopo wa kisiasa (Political Stability).


Balozi Nguyen Nam Tien ameelezea uhusiano wa Tanzania na Vietnam kuwa ni wa muda mrefu zaidi ya miaka 56 iliyopita ambapo ulianzia kwenye mambo ya siasa lakini ukiendelea mpaka hivi sasa ambapo nchi hizo mbili zina mashirikiano karibu kwenye sekta mbalimbali.


Mhe. Balozi amesema kwamba Vietnam inajitahidi kuwekeza kwenye masuala ya Kilimo na viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo.


Aidha, Mhe. Balozi amesema kwamba asilimia 60% ya wananchi wa Vietnam wanajishughulisha na kilimo. Mazao Makubwa ya kilimo ni mpunga, kahawa, korosho pamoja na Ufugaji wa samaki.


MWISHO

No comments:

Post a Comment