Thursday, June 10, 2021

WAKULIMA WAPONGEZA MPANGO WA KILIMO CHA UMWAGILIAJI.

Na Swaum Katambo, Tanganyika-Katavi

Wakulima katika Kijiji cha Majalila Kata ya Tongwe Wilayani Tanganyika Mkoani Katavi wameishukuru Serikali kwa Mpango wa kuboresha Miundombinu ya umwagiliaji na kusema kuwa itawasaidia kufanya Kilimo chenye tija tofauti na wanavyolima kwa kutegemea mvua za Msimu.

Wamesema hayo mara baada ya kusikiliza Hotuba aliyoitoa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Mwigulu Nchemba kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 katika Sekta ya Kilimo kuwa Maeneo yatakayopewa msukumo ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji.

"Kwa bajeti ya leo inaonekana wakulima inatuinua, Serikali imetuangalia kwa macho mawili labda tusubiri utekelezaji kwa sababu yanayosemwa ni mazuri lakini kwenye utekelezaji sasa inaweza isifanye vizuri", Alisema Ramadhan Nyembe Mkulima Kijiji cha Majalila.

Nyembe ametolea mfano kwa Mkoa mzima wa Katavi kuwa una Skimu za Umwagiliaji tatu huku skimu hizo zikiwa hazijakamilika hivyo anaamini kuwa Serikali ikitilia mkazo katika Kilimo cha umwagiliaji na kuzikamilisha Skimu hizo wakulima watalima Kilimo chenye tija.

Hata hivyo wakulima pia wameipongeza hatua ya Serikali kutaka kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo zana za kilimo, mbegu bora za mazao, mbolea na viuatilifu. 

"Zamani tulikuwa tunanunuliana tuu una debe la Malamata uniletee hapa,basi tunapanda tuu kienyeji..,lakini upatikanaji wa mbegu bora za mazao itakuwa na kipato kingi cha kutosha tofauti na tulivyozoea mwanzoni" Alisema Emmanuel Ramadhan Mkulima mdogo.

Aidha, wakulima katika Kijiji cha Majalila wameiomba Serikali kuwasogezea nyenzo au kuwapatia vifaa kwa ajili ya kuvunia mazao kwani wanapata Changamoto nyingi pindi unapofika msimu wa mavuno.

"Kama unavyoona hivi tunahangaika sana,lakini tungekuwa tunatumia mashine tungekuwa tumeshamaliza muda mrefu,tunaomba sana Serikali ituangalie hata kwa kutupa Mikopo ya Vitendea kazi tungeshukuru sana" Alisema  Nyembe.

Kwa Mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha Bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 amesema Serikali ina Mpango wa kuongeza matumizi ya teknolojia na mbinu za kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi,
kuongeza matumizi ya teknolojia bora katika uzalishaji wa mazao ili kuongeza uzalishaji na tija, kuimarisha vituo vya utafiti wa mbegu bora,vyuo vya mafunzo na vituo vya mafunzo ya wakulima na huduma za ugani. 

Kadhalika, Serikali inatarajia kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi,Vilevile itaendelea kuhamasisha uzalishaji wa mazao yakiwemo mazao ya kimkakati ya Mkonge, Chikichi, Tumbaku,Pareto,Korosho, Kahawa na Pamba. 

MWISHO

No comments:

Post a Comment