Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,akizungumza katika uzinduzi wa Magari yanayotumia Gesi Asilia,uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Juni 25, 2021.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, akizungumza katika uzinduzi wa Magari yanayotumia Gesi Asilia,uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Juni 25, 2021.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,akikata utepe kuashiria kwa uzinduzi wa Magari yanayotumia Gesi Asilia,uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Juni 25, 2021.(Katikati )Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Petroli Tanzania(TPDC) Dkt. James Mataragio(kulia)Kamishna Msaidizi wa Gesi Mhandisi Mohamed Fakihi.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akimkabidhi mfano wa ufungo wa gari, Ndugu Seif Ally Seif(katikati) mara baada ya kuzindua uzinduzi wa wa Magari yanayotumia Gesi Asilia,uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Juni 25, 2021.
Matukio kwenye uzinduzi wa Magari yanayotumia Gesi Asilia,uliofanyika Jijini Dar es Salaam, Juni 25, 2021.
Hafsa Omar-Dar es Salaam
Imeelezwa kuwa,Tanzania inaongoza kwa kuwa na Rasimali ya Gesi asili nyingi kuliko nchi nyengine za Afrika Mashariki.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, Juni 25, 2021 wakati wa uzinduzi wa magari yanayotumia Gesi Asilia,uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika uzinduzi huo,Dkt. Kalemani ameeleza kuwa kwasasa nchini kuna gesi nyingi ya kutosha kulinganisha na nchi za jirani, ambapo amebainisha kuwa tayari kuna gesi ya futi za ujazo trilioni 57.54 na bado shughuli za utafutaji na undelezaji wa gesi zinaendelea.
Aidha, amesema Serikali imeshasambaza gesi katika sehemu mbalimbali nchini,amezitaja sehemu hizo ambazo ni viwandani, manyumbani na kwenye magari ambapo ameeleza gari iliyozinduliwa ni gari ya 701 kuwekewa gesi nchini.
Dkt. Kalemani amewataka watanzania kuanza kununua magari yenye mfumo wa kuweka gesi na kuwataka wenye magari ambayo yanatumia mafuta kubadilisha mfumo huo na kuweka mfumo wa kutumia gesi kwakuwa vituo vya kubadilisha mfumo huo vipo nchini.
Amevitaja vituo hivyo vya kuweka mfumo wa kutumia gesi, ni kituo cha Chuo kikuu cha Dar es Saalam na DIT, na kuwasisitiza watanzania watumie gesi kwakuwa gesi haina gharama na pia inapunguza uharibifu wa mazingira.
Pia, amewataka TPDC, GASCO,pamoja na wenye vituo kuangalia upya bei ya kubadilisha mfumo huo ili Watanzania wengi waweze kubadilisha gari zao kutoka kwenye mfumo ya kutumia mafuta kwenda kwenye mfumo wa kutumia gesi.
Waziri Kalemani,amewatoa wasiwasi Watanzania kuhusu upatikanaji wa vituo vya kujazia gesi, ambapo amefafanua kuwa kuna vituo vitano vinajengwa na tayari vituo viwili vya kuwekea gesi vinatoa huduma hiyo kituo cha Ubungo na Chuo kikuu cha Dar es Saalam.
“Tumetoa maelekezo kwa wataalamu wetu,mwakani tutaweka vituo vingi karibu kwa kila jiji tutaweka kituo cha kujaza gesi katika magari, tunaanza na Dodoma,Mbeya,Tanga na Arusha na tutakuwa na vituo vidogo vidogo tunataka tuwe na vituo vya kujazia gesi sawa na vituo vya mafuta,”alisema.
Vilevile, ametoa wito kwa wawekezaji wengine kujitokeza kwa wingi kutumia rasilimali ya gesi asilia kwakuwa gesi bado ipo nyingi na haijatumika kwa kiwango kikubwa amewataka kutumia gesi hiyo ili kuchochea shughuli za kiuchumi hapa nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kufanya uwekezaji mkubwa wa ugunduzi na uwekezaji wa Gesi asilia na kuifanya nchi iweze kusikika katika uwekezaji wa gesi.
Amesema kuwa, anatarajia kuona wawekezaji wengi nchini Tanzania wenye viwanda na makampuni mbalimbali hasa wenye magari kuanza kutumia magari yenye mfumo wa kujazia gesi ili kupunguza uharibifu wa mazingira.
Waziri Jafo, amemuagiza mtendaji mkuu wa NEMC kuhakikisha kuwa hakuna kituo chochote cha mafuta kinachowezwa kujengwa lazima kipate kibali cha tathmini ya mazingira na sharti moja la kupata kibali hiko kuanzia mwezi julai lazima muwekezaji yoyote katika kituo chake aweke eneo ambalo atafunga mtungi wa gesi.
Nae, Seif Ally Seif, ambae mmiliki wa gari lililozinduliwa amesema magari ya Scania mapya yanayotumia gesi asilia yataleta mapinduzi makubwa katika uchumi wa nchi kwakuwa sio tu yataokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika katika kuagiza mafuta nje, lakini yatasaidia kuongeza pato la Taifa kutokana na kuwa yatatumia gesi ambayo inazalishwa nchini.
No comments:
Post a Comment