Tuesday, June 15, 2021

SERIKALI KUENDELEZA MKAKATI KUTOKOMEZA UKATILI NA MAUAJI YA WAZEE

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwanaidi Ali Khamis akizungumza na Wazee na wadau wa Mashirika yanayotetea Haki za Wazee katika maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee yaliyofanyika leo Juni 15, 2021 jijini Dodoma.

Katibu Mkuu WIzara ya Afya- Idara Kuu ya Mmaendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akieleza namna Wizara inavyoshirikana na wadau katika kuhakikisha Wazee wanalindwa nchini maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee yaliyofanyika leo Juni 15, 2021 jijini Dodoma

 

Baadhi ya Wazee na wadau wa Mashirika yanayotetea Haki za mzee wakisikiliza hotuba ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwanaidi Ali Khamis katika maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili dhidi ya Wazee yaliyofanyika leo Juni 15, 2021 jijini Dodoma

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Mwanaid Ali Khamis ameseme kuwa serikali imeazimia kuendeleza utekelezaji wa mkakati wa kutokomeza ukatili na mauaji ya wazee nchini.

Ameyabainisha hayo leo Juni 15,2021 jijini Dodoma wakati alipokuwa akitoa hotuba ya ufunguzi wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kupinga ukatili dhidi ya wazee.

Amesema kuwa katika kutimiza azma ya kuendelea kuwalinda wazee pamoja na kuimarisha huduma nyingine, serikali ipo katika hatua za mapitio ya sera ya Taifa ya wazee ya 2003, ambayo inaweka msisitizo katika kuimarisha upatikanaji wa haki ya ulinzi na usalama kwa wazee.

Aidha, amesema kuwa sera inayofanyiwa mapitio inalenga kuimarisha mifumo ya ulinzi shirikishi katika jamii ya kuwalinda wazee kutokana na hatari ya kufanyiwa vitendo vya ukatili, pamoja na mifumo ya upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya wazee.

“Kutokana na ukweli kwamba hali duni ya kipato ni miongoni mwa sababu zinazochangia vitendo vya ukatili kwa wazee, serikali inalenga kuhakikisha wazee wanawezeshwa katika kubuni na kuendesha shughuli za ujasiriamali kupitia vikundi vidogo vidogo katika jamii ili kuwawezesha kuinua kipato na kumudu mahitaji yao ya msingi”amesema

Pia, amesema kuwa wazee watawezeshwa kushiriki katika shughuli za michezo na burudani ili kuimarisha afya zao na kuwajenga kisaikolojia.

Amesema, katika jitihada hizo za kuimarisha ulinzi kwa wazee, serikali kwa kushirikiana na wadau inaendelea na mapambano ya kutokomeza vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee kwa kuongeza msukumo na kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa Mkakati wa kitaifa wa kutokomeza mauaji ya wazee kwa kipindi cha miaka mitano (2018/2019-2022/2023).

Hata hivyo, amesema kutokana na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau, vitendo vya ukatili na mauaji ya wazee nchini vimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa.

“Kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi la Polisi, mauaji ya wazee yamepungua kwa kiwango kikubwa kutoka 577 mwaka 2014 hadi wazee 34 Desemba 2020”amesema

Vilevile, amesema kuwa serikali inadhamiria kuongeza jitihada na kuhakikisha mauaji ya wazee yanakwisha kabisa.

“Serikali katika mapitio ya sera ya wazee ya mwaka 2003 imezingatia kuweka msisitizo zaidi katika kuhakikisha wazee wanapata huduma ya msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha ili kusaidia kuimarisha afya na ustawi wao”amesema

Amesema kuwa kwa mujibu wa mwongozo wa kitaifa wa Utoaji wa Huduma za Msaada wa Kisaikolojia wa Mwaka 2021, matatizo mengi ya kiafya na kimahusiano yanayowakabili wazee yanatibika kikamilifu kupitia msaada wa kisaikolojia na ushauri nasaha.

Kadhalika amesema kuwa kupitia Mpango wa serikali wa kuboresha huduma za afya, imeendelea kuhakikisha kuwa kila kituo cha afya na hospitali zinakuwa na madirisha maalum kwa ajili ya matibabu kwa wazee.

“Mpaka sasa kuna jumla ya madirisha 2,335 mahususi kwa ajili ya kutolea huduma za matibabu kwa wazee”amesema

Meneja Program, haki na ushirikiano wa wadau kutoka shirika la Help Age Intrnational Tanzania, Joseph Mbasha amesema kuwa shirika hilo ni miongoni mwa mashirika mtandao yaliyopigania utambulisho huo na lina dira ya kuona dunia ambayo kila mzee anaishi maisha yenye afya, hadhi na usalama.

“Shirika linaamini kuwa kwa kukuza ustawi haki na ujumuishi wa wazee wataweza kuishi maisha yenye afya, hadhi na salama”amesema Mbasha

Amesema katika kutekeleza azma hiyo shirika hilo linatekeleza afua tano, ambazo ni kuboresha upatikanaji wa huduma za afya zilizo rafiki na bora kwa wazee.

Amesema afua nyingine ni kupinga vitendo vya ukatili na manyanyaso dhidi ya wazee, kutoa huduma jumuishi wakati wa majanga, kuhakikisha usalama wa kipato, pamoja na kuchagiza harakati za mabadiliko.

No comments:

Post a Comment