Mkuu wa Mkoa wa
Songwe, Omary Mgumba akizungumza wakati akizindua mkutano wa 11 wa wadau wa
Kahawa Nchini jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa
Bodi ya Kahawa Nchini, Prof Aurelia Kamuzora akizungumza katika ufunguzi wa
mkutano wa 11 wa wadau wa kahawa Nchini unaofanyika jijini Dodoma.
Wadau wa zao la
kahawa wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Nchini, Prof Aurelia Kamuzora
akizungumza kwenye ufunguzi wa kongamano la wadau wa zao hilo unaoendelea
jijini Dodoma.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo_dodoma
WADAU wa zao la Kahawa wametakiwa kutumia uzoefu wao na weledi katika kuhakikisha kuwa sekta ya Kahawa inabadilika kwa kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa zao hilo.
Wito huo umetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba wakati akifungua
Mkutano wa 11 wa wadau wa kahawa jijini Dodoma ambapo amesema wana jukumu kubwa
la kuhakikisha zao hilo linakua.
RC Mgumba amesema zao la kahawa ni mojawapo ya mazao ya kimkakati
yaliyochaguliwa na Serikali hivyo yanapaswa kubadilika na kukua ili yaweze
kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Nchi sambamba na kuwa
mwarobaini wa ajira kwa vijana.
Amesema kwa sasa uzalishaji wa zao hilo Siyo mzuri hivyo wadau hao wanapaswa
kutumia kongamano hilo ili liweze kuwasaidia kujadili changamoto zinazolikabili
zao hilo na kutoka na mawazo ya pamoja ya namna gani wanaweza kulikuza na kuwa
msaada kwa Taifa.
" Kahawa nayo ni mojawapo ya mazao ya kimkakati kwa Nchi yetu, linatakiwa
kukua na kutoa mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wetu, kama tutatumia
mkutano huu vizuri kupata majibu ya changamoto zinazolikabili zao hili basi
naamini tunaweza kuifanya Kahawa kuwa mojawapo ya kilimo kitakachoajiri kundi
kubwa la vijana.
Tutumie kongamano hili kila mmoja kwa uwezo, taaluma na uzoefu wake kujadiliana
kwa pamoja kutatua changamoto hii ya uzalishaji mdogo hata kule kwangu Songwe
uzalishaji umeshuka siyo kama zamani," Amesema Mgumba.
RC Mgumba ametaja changamoto zinazoikabili sekta ya kahawa kuwa ni pamoja na
tija ndogo, uzalishaji mdogo, kuyumba kwa bei ya kahawa katika soko la Taifa,
ukosefu wa mitaji kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kushindwa kukopesheka kwenye
taasisi za fedha ambayo yote yanalifanya zao hilo kuonekana halilipi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Nchini, Prof Aurelia Kamuzora
amezungumzia umuhimu wa zao hilo huku akisema limemsaidia yeye binafsi kwenye
maisha yake na kutoa rai kwa wadau wa kahawa kuungana kwa pamoja kukuza kilimo
hiko.
Mkutano huo wa 11 wa wadau wa kahawa unafanyika kwa siku mbili jijini Dodoma
ambapo unawakutanisha wadau wa kahawa kutoka maeneo tofauti ambapo linakwenda
sambamba na kauli mbiu isemayo " Uzalishaji wenye tija ndio nguzo ya
maendeleo ya sekta ya kahawa"
MWISHO
No comments:
Post a Comment