Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) Philemon Bagambilana.
Mwakilishi wa Katibu Mtendaji wa Shirika la Uwezeshaji wa Usafiri wa Ushoroba wa Kati (CCTTFA) Costaph Natay akitoa nasaha zake kwa watumishi waliopatiwa mafunzo ya awali ya ubaharia (hawapo pichani).
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya MSCL Dkt. Tumaini Gurumo akimkabidhi cheti cha kuhitimu mafunzo ya awali ya ubaharia mtumishi wa MSCL Evodius Nkulanga (kulia).
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya MSCL Dkt. Tumaini Gurumo (wa tatu kutoka kulia waliokaa) akiwa na watendaji wengine wa Kampuni hiyo, katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi waliohitimu mafunzo ya awali ya ubaharia na kuwapatia vyeti.
Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya MSCL Dkt. Tumaini Gurumo akiongea na watumishi 49 waliopatiwa mafunzo.
Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) kupitia ufadhili wa Shirika la Uwezeshaji wa Usafiri wa Ushoroba wa Kati (CCTTFA) wamefanikiwa kutoa vyeti kwa watumishi 49 waliomaliza mafunzo ya awali ya Ubaharia yatakayowawezesha watumishi hao kuendesha na kusimamia shughuli za melini pamoja na kutatua changamoto za abiria wawapo safarini.
Mafunzo hayo ya wiki tatu yaliyofanyika katika awamu tatu tofauti ikiwemo awamu mbili zilizojumisha watumishi pamoja na mafunzo maalum ya memeneja na maafisa waandamizi wa Kampuni hiyo yaliyokusudia kuwajengea uwezo katika uendeshaji na usimamizi wa mashirika ya usafirishaji kwa njia ya maji.
Akizungumza kabla ya Mgeni rasmi wa hafla hiyo fupi ya kuwakabidhi vyeti watumishi waliohitimu mafunzo hayo tarehe 17.6.2021 shughuli iliyoambata na ufunguzi wa mafunzo maalum kwaajili ya Mameneja wa Kampuni, Kaimu Mtendaji Mkuu wa MSCL Philemon Bagambilana aliwaomba watumishi wa Kampuni hiyo kuthamini na kuheshimu ufadhili uliotolewa na CCTTFA ili kuleta tija katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.
“MSCL ni taasisi ambayo inakuwa na mnajua katika mpango mkakati wetu tunategemea ikifika mwaka 2026 tutakuwa na meli si chini ya 22 na wafanyakazi wataongezeka kwahiyo haya mafunzo ni ya kudumu na ni endelevu na mnakumbuka technolojia inazidi kukua, basi niwashukuru wale ambao mmehitimu na niwapongeze pia lakini tuendelee kuwa na moyo huo huo wa kujifunza na kuwa mabalozi wazuri”, Alisema.
Aidha, Mwakilishi wa Katibu Mtendaji wa CCTTFA Costaph Natay aliushukuru uongozi wa MSCL kwa kuwaalika kushuhudia hafla ya utiaji saini wa mikataba mitano ya ujenzi wa meli nne na ukarabati wa meli moja iliyofanyika mebele ya Rais Samia Suluhu Hassna tarehe 15.6.2021 na kusisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza chachu ya kuimarisha biashara ya usafirishaji kati ya nchi yetu na nchi zisizokuwa na mlango wa bahari na kuongeza kuwa ukarabati huo ni vyema ukaenda sambamba na mafunzo ya uendeshaji wa meli hizo.
“Mtendaji Mkuu amesema kuwa ana deni kubwa lakini nimkumbushe kuwa sisi kuwawezesha MSCL kwenye mafunzo na sisi tunanufaika vile vile, kwasababu ni wajibu wetu sisi kama Ushoroba wa Kati kuhakikisha kwamba nchi ambazo hazina mlango wa bahari zinatumia hii njia ya ushoroba wa kati, maana yake ni kwamba wananchi wa DR Congo, Burundi na Uganda wanategemea huu ukanda wa kati, kwahiyo mnavyoongeza ufanisi wenu kwenye Ziwa Tanganyika au Ziwa Victoria mnatusaidia kutimiza malengo tuliyopewa kama taasisi,” Alisisitiza.
Akitoa taarifa ya mafunzo hayo Afisa utumishi wa MSCL Baraka Bigambo alisema kuwa makubaliano maalum (MoU) yaliyosainiwa kati ya MSCL na CCTTFA tarehe 16, Januari, 2021. CCTTFA iliridhia kufadhili mpango wa mafunzo kwa watumishi wa Kampuni hiyo hususana wenye kada ya ubaharia na mameneja.
Kwa upande wake Mgeni rasmi wa Hafla hiyo Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya MSCL Dkt. Tumaini Gurumo aliwasisitiza watumishi waliopata mafunzo hayo kuhakikisha wanakuwa na nidhamu katika kazi na kuwa matunda ya elimu waliyopatiwa yanajionesha kwa vitendo na vile vile aliridhishwa na shauku ya mameneja wanaoendelea na mafunzo yao ya usimamizi wa mashirika ya usafirishaji kwa njia ya maji yanayotarajiwa kumalizika 25.6.2021.
“Tunategemea sasa tuione MSCL mpya, taasisi yetu imekuwa kwa muda mrefu sana inaendeshwa kwa namna ambavyo imekuwa ikiendeshwa lakini imekuwa na uhaba mkubwa sana wa ‘professionalism’ (utaalamu), utambuzi uweledi wa masuala ya ‘Shipping’, sasa hii elimu tunayoipata ambayo ni mwanzo naiita ‘eye opening’ itusaidie sisi kuona wapi tumepungua kwasababu fursa ipo na niwapongeze sana CCTTFA kwamba wao wametimiza wajibu wao sasa sisi mpira upo miguuni kwetu tunauchezaje? Sitegemei MSCL ikumbatie mpira, nategemea elimu hii na ujuzi huu tulioupata utuletee tija katika taasisi hii,” alimalizia.
Akitoa salamu zake za shukran Mkuu wa Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam Dkt. Erick Msami aliwataka watumishi hao kutoangusha jitihada za serikali kwani serikali imeamua kuwekeza mabilioni ya fedha kwa MSCL ili kuhakikisha kuwa inaendesha shughuli zake na hartimae kuwarahisishia wananchi usafiri wa majini.
“Kwa kupitia mafunzo haya tunayoendelea kuyapata, naamini yatatusaidia, tutaendelea kusimamia shughuli hizi kwa ufanisi na miradi tutaisimamia vizuri na itakapokamilika tutahakikisha kwamba tunakuwa na taswira nzuri mbele ya watanzania,” alieleza.
Ufadhili huo mafunzo uliogharimu shilingi Milioni 209 ni utekelezaji wa takriban asilimia 40 tu ya Mkataba huo maalum uliosainiwa mwanzoni mwa mwaka 2021.
No comments:
Post a Comment