Sunday, May 2, 2021

WAZIRI BASHUNGWA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA BASATA, BODI YA FILAMU NA COSOTA


Na Mathias Canal, WazoHuru Media


Sheria/Kanuni iliyopo inayotaka BASATA, BODI ya FILAMU kujiridhisha kwa njia ya kufanya uhakiki imelenga kusimamia maudhui ya sanaa ili yasiende kinyume na mila, desturi na utamaduni.


Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe Innocent Bashungwa ameyasema hayo leo tarehe 2 Mei 2021.


Hata hivyo, ameliagiza Baraza la Sanaa Tanzania-BASATA, BODI ya FILAMU na Chama Cha Hakimiliki Tanzania-COSOTA kufanya uhakiki kwa utaratibu ambao haukwamishi kazi za wasanii nchini.


Bashungwa amesema kuwa Uhakiki huo unakusudia kulinda maadili hasa ya watoto kwa kuhakikisha maudhui mabaya hayawafikii. 


Ameongeza kuwa Kwa upande wa filamu, uhakiki unasaidia kujua maudhui yaliyopo kwenye filamu husika ili kuamua ipangiwe daraja gani. 


Ameongeza kuwa Uhakiki pia unasaidia kuepusha maudhui mabaya ya kuharibu maadili ya jamii ili yaweze kudhibitiwa kabla ya kufika kwa mtazamaji/msikilizaji hasa watoto wadogo.


Waziri Bashungwa amesema kuwa Ili kusimamia vyema malengo hayo ya kulinda maadili ya jamii bila kuathiri ubunifu wa wasanii, maendeleo ya sanaa nchini, na kudumaza ukuaji wa ajira; Wizara inafanya uchambuzi ili kuona kama kuunganishwa kwa BASATA na BODI ya FILAMU kunaleta tija, weledi na ufanisi katika kuhudumia wadau na kusaidia ukuaji wa tasnia. 


Amesema kuwa hilo linaenda sambamba na kupitia sera, sheria na kanuni mbalimbali zinazosimamia tasnia na taasisi hizo.


Aidha, Amesema Wizara imeishapata baadhi ya maoni ya wadau na hivyo ametoa mwito kwa wadau ambao hawajawasilisha maoni yao kufanya hivyo. 


Hali kadhalika, Kama Waziri mwenye dhamana, pamoja na watumishi wote Wizarani wataendelea kukutana na wadau ikiwa ni sehemu ya namna ya kuboresha chambuzi na hoja zilizowasilishwa. 


"Kwa pamoja tushirikiane kujenga tasnia ya habari, sanaa, michezo na urithi wa utamaduni wetu ili kuendelea kuwa na Taifa Imara" Amesisitiza Waziri Bashungwa


MWISHO

No comments:

Post a Comment