Waziri wa Viwanda na
Biashara, na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo akifafanua jambo
katika mkutano wa Baraza la kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na
Uwekezaji (SCTIFI) kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki leo
jijini Arusha. Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.
Geofrey Mwambe. Kulia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda - Zanzibar,
Mhe. Omar Said Shaaban. Picha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki
Ujumbe wa Uganda ukifuatilia
mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji
(SCTIFI)
Waziri wa Viwanda na Biashara
kutoka Kenya, Mhe. Betty Maina akiwasilisha hoja kwenye mkutano wa Baraza la
Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI). Kulia ni
Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya
Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote
Ujumbe wa Kenya ukifuatilia
mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji
(SCTIFI)
Ujumbe wa Rwanda ukifuatilia mkutano Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI)
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Baraza la Kisekta la Mawaziri
wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika
Mashariki lakubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara na kuimarisha
biashara na uwekezaji ndani ya Jumuiya hiyo.
Awali akifungua mkutano
Ijumaa Jijini Arusha, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi
Steven Mlote amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwani utawawezesha mawaziri
kupitia na kujadili miongozo ambayo itasaidia kuboresha biashara katika ukanda
wa Afrika Mashariki ikiwemo kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara.
Aidha, Mhandisi Mlote
ameongeza kuwa, kwa kuzingatia kanuni na sheria ya Afrika Mashariki, vikwazo
visivyo vya kibiasha baina ya nchi na nchi vimekuwa vikizuia ukuaji wa biashara
hivyo ni muhimu kupitia mkutano wa baraza la mawaziri kuangalia namna ya
kuviondoa ili kuwezesha ukuaji wa biashara ndani ya jumuiya.
Nae Waziri wa Viwanda na
Biashara, na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa
mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana mambo mengi ya msingi
ikiwemo kuendelea kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kikodi.
“Tumezungumza pia kuhusu
ushiriki wetu katika kufanya biashara na Uingereza kwa kuzingatia kuwa
Uingereza siyo sehemu Jumuiya ya Ulaya, lakini pia tumezungumzia suala la EAC
kujiunga na jumuiya ya biashara ya Afrika ambayo sisi Tanzania tupo katika
hatua kadhaa na kuona kuwa na sisi tunajiunga na jumuiya hiyo mwaka huu,”
Amesema Prof. Mkumbo
Kwa upande wake, Waziri wa
Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe amesema kuwa mawaziri
wamekubaliana kutoa msukumo wa biashara katika jumuiya ya afrika mashariki lizingatiwe
na kupea kipaombele na kuruhusu sekta binafsi kufanya biashara katika nchi
mbalimbali.
“Pamoja na mambo mengine, pi
tumekubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kiushuru (Non-tarrif barriers)
viondolewe kwani vimekuwa vikikwamisha biashara bila sababu za msingi, na
kuangalia jinsi ya kuwekeza kwenye eneo la uwekezaji ndani ya jumuiya ya Afrika
Mashariki kwa kuwa na mikakati ya pamoja ya kuvutia wawekezaji” amesema Mhe.
Mwambe
Miongoni mwa maeneo
yaliyojadiliwa ni pamoja na maamuzi ya ripoti ya mawaziri wa fedha, ripoti ya
kamati ya forodha, ripoti ya kamati ya biashara, ripoti ya kamati ya viwango ya
Afrika Mashariki, ripoti juu ya masuala ya ushindani pamoja na ripoti ya kamati
ya uwekezaji.
Mkutano huo umehudhuriwa na
Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Kenya Mhe. Betty Maina, Waziri wa Viwanda
na Biashara, - Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Geofrey Mwambe,
Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda - Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban.
Wengine ni Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Mhe. Beata Habyarimana, Waziri wa Biashara, Viwanda na Ushirika wa Uganda, Mhe. Grace Choda, pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara, Uchukuzi, Viwanda na Utalii wa Burundi, Balozi Jeremie Banigwaninzigo.
No comments:
Post a Comment