Wednesday, April 14, 2021

TANZANIA TUPO VIZURI LAKINI TUSIBWETEKE TUENDELEE KUJIKINGA NA CORONA



Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,Wazee na Watoto Dk. Leonard Subi amesema kuwa Tanzania ni mojawapo Kati ya nchi zinazochukua tahadhari kubwa sana ya kupambana na magonjwa ya milipuko kama Corona.

Aliyasema hayo wakati akifungua kikao cha siku tatu kinachofanyika Jijini Arusha kilichoshirikisha wataalam mbalimbali, mashirika binafsi na wadau wa Afya  nchini.
"Tanzania tuko salama na wananchi wetu waendelee na maisha kama kawaida" alisema Dr. Subi.

Vilevile Dr. Subi ameendelea kusisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari zote za ugonjwa wa Corona ikiwemo utamaduni wa kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni, kuvaa barakoa kwa usahihi na kuepuka misongamano isiyo ya lazima. 

Aidha Dr. Subi ametoa wito wa kuendelea kuyalinda makundi ya watu walio katika hatari ya kuathiriwa zaidi na ugonjwa wa Corona ikiwa ni makundi ya wazee pamoja na watu wenye magonjwa sugu kama Kisukari na presha.

Zaidi Dr. Subi ameweka msisitizo kwa watanzania kuzingatia mtindo bora wa maisha ikiwa ni pamoja na kuzingatia mazoezi ya mwili na viungo na kuzingatia lishe bora ili kuongeza kinga za mwili katika kupambana maradhi ya kuambukiza pamoja na yale yasiyoambukiza.

No comments:

Post a Comment