Thursday, April 8, 2021

SURA 3 ZA RAIS SAMIA


Na Emmanuel J. Shilatu

Tangua aapishwe kuwa Rais wa awamu ya 6 wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameonyesha sura kuu 3 zinazotoa mwelekeo wa kiutendaji kwake.

*A: UHODARI NA TUMAINI*

Rais Samia amepokea kijiti cha Urais kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa 5 wa Tanzania Hayati Dkt John Magufuli na wa kipindi chote ameliongoza vyema Taifa kwa uhodari wa ufariji kwa Watanzania wote. Rais Samia amewafariji wafiwa upande wa familia, amewafariji Watanzania na kujawa faraja, tumaini na nguvu mpya.

Rais Samia ameonyesha uhodari katika ulezi ambapo amesimama kama Mama ndani ya uongozi kwa kuwapa onyo, angalizo ambalo ni sawa na kuwapa fursa nyingine ya kujisahihisha ili safari ijayo vijana wakizingua basi Mama atawazingua vyema.

Rais Samia ameonyesha namna alivyo komaa kiuongozi kwa kusimamia vyema utawala wa sheria kwa kuwasimamisha wenye tuhuma kwanza kupisha uchunguzi na sio kuwatimua moja kwa moja pasipo kutoa nafasi ya kumsikiliza ili kubaini ukweli wa tuhuma. Huyo ndio Mama yetu Rais Samia.

Rais Samia ameanza kwa kutoa agizo vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe. Nyota njema ya uendelezwaji wa uhuru wa habari nchini uliokuwapo miaka na miaka.

*B: UZALENDO*

Rais Samia ameonyesha uzalendo wa kuzilinda rasilimali zetu nchini kama ambavyo mtangulizi wake Hayati Dkt Magufuli amefanya.

Mathalani, Rais Samia amekemea utoroshwaji na uchimbaji kiholela wa madini ya Tanzanite kwenye machimbo ya mererani. Ni mwanzo mzuri wa kuhakikisha madini tuliyobarikiwa yanatunufaisha Watanzania.

*C: UCHAPA KAZI*

Katika kuonyesha zege halilali, Rais Samia ndani ya muda mfupi amefanya teuzi na tenguzi mbalimbali za viongozi na kuwaapisha.

Pia ametoa mwelekeo wa Serikali yake; kazi ya utekelezaji ilani ya uchaguzi inaendelea;  ameendeleza urithi wa miradi ya kimkakati ya kimaendeleo aliyoiacha Hayati Dkt Magufuli.

Itoshe kusema kazi inaendelea kupitia sura 3 za uchapa kazi, uzalendo na uhodari wa Rais Samia.
 
Ndugu zangu, Tuendelee kunywa mtori, nyama tumezikaribia.
*Shilatu, E.J*

No comments:

Post a Comment