Mkuu wa mkoa Ruvuma Chistina Mndeme amewaagiza wakuu wa Taasisi serikalini kusikiliza na kutatua kero za wananchi kuanzia ngazi ya chini.
Mndeme ametoa kauli
hiyo katika kikao cha kazi cha watendaji na wakuu wote wa Taasisi za serikali mkoani Ruvuma kilichofanyika katika ukumbi
wa Manispaa Songea.
“Mimi kama Mkuu wa
Mkoa nimekuwa nikipokea kero mbalimbali ambazo wakati mwingine kero hizo
zingetatuliwa katika ngazi ya wilaya au kijiji,nimeona ni vema niwaite wakuu wa
Taasisi zote, kwa sababu tunapaswa kutatua kero za wananchi kwenye maeneo yetu’’,alisisitiza.
Amewaagiza watendaji
hao kusikiliza kero za wananchi kwa wakati na kuwaagiza kutosubiri kero
kuwafikia ofisini badala yake waweke ratiba ya kwenda kwa wananchi kusikiliza
kero zao na kuzipatia ufumbuzi kwa wakati.
Mndeme ameagiza kila
Halmashauri na Taasisi kuunda mkakati wake wa kushughulikia kero za wananchi
ili kupunguza kero hizo kuanzia ngazi ya chini.
“Sasa hivi tuna
tatizo la mara kwa mara la kukatika kwa umeme,wewe Meneja wa TANESCO kazi yako
ni nini,watu wamelipia umeme,hawajaunganishiwa umeme,wewe kama Meneja wa
TANESCO kwanini huendei kwa wananchi na
kutoa sababu za kero hizo,tutoe taarifa kwanini maji yamekatika,sio mimi Mkuu
wa Mkoa nikatoe taarifa kwa wananchi,tuwasiliane na wananchi’’, alisema Mndeme.
Hata hivyo Mkuu wa
Mkoa amezitaja sababu mbili kubwa zinaosababisha kero kwa wananchi ni
kutokufanyika vikao vya kisheria na wananchi
na kutokuwepo kwa mahusiano mazuri miongoni mwa watendaji wa serikali
hivyo ameagiza kufanyika kwa vikao vya kisheria na kuimarisha mahusiano ndani ya Taasisi za
serikali ambayo yatasaidia kupunguza kero kwa wananchi.
“Tukitekeleza
majukumu yetu vizuri kwa wananchi,tutaifanya kazi ya Mheshimiwa Rais wetu Samia
Suluhu Hassan kuwa nyepesi,sisi ndiyo tupo chini,tutoke maofisini,tusisubiri
ziara ya Mkuu wa Mkoa,ninyi wakuu wa Taasisi mnaruhusiwa kwenda kuzungumza na
wananchi na kutatua kero zao’’,alisisitiza.
Mndeme ameagiza kila
Taasisi kuandaa rejesta ya malalamiko ya ambayo itaratibu malalmiko pia kuunda
timu ndogo itakayosaidia kuratibu malalamiko na kuyafikisha kwa mkuu wa Taasisi
na kwamba kero za kisera zipelekwe ngazi ya juu ili ziweze kupata utatuzi wa
kisera.
Ili kuhakikisha
utatuzi wa kero unakuwa endelevu,Mkuu wa Mkoa ameziagiza Taasisi za serikali
kila mwisho wa mwezi kufanya tathimini namna kero zilivyoshughulikiwa na kutoa
taarifa za kero zinazohitaji ufafanuzi wa kisera kwa wananchi.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wa Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho amesema ilani ya CCM ya 2020/ 2025
inalitaja moja ya jukumu lake ni kusikiliza malalamiko ya wananchi hivyo jambo
linalofanywa na uongozi wa mkoa wa
Ruvuma ni utekeleza wa ilani.
Naye Mkuu wa Wilaya
ya Tunduru Julius Mtatiro amesema katika kushughulikia malalamiko ya wananchi na
kwamba hakuna mfumo wa pamoja,hali inayosababisha wananchi kutojua wakimbilie
wapi katika kupata suluhu ya matatizo yao.
Ili kuhakikisha kero
za wananchi zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu,Mkoa wa Ruvuma umeazimia kuunda timu
ya Mkoa ya kutatua kero zinazowakabili wananchi ambayo itakutana kila baada ya
miezi mitatu.
No comments:
Post a Comment