Wednesday, April 14, 2021

Nabii Joshua:Nitaendelea kusimama imara kumuombea Rais Samia

Rais wa New Covenant Unity International (NCUI) ambaye pia ni Kiongozi wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala akionyesha cheti baada ya kutunukia udaktari wa heshima mjini Kibaha mkoani Pwani na Profesa Benezer David wa huduma ya All Nations Christian Church International kutoka Amarilo nchini Marekani.

Profesa Benezer David wa huduma ya All Nations Christian Church International kutoka Amarilo nchini Marekani akimtunuku cheti cha udaktari wa heshima Rais wa New Covenant Unity International (NCUI) ambaye pia ni Kiongozi wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala leo mjini Kibaha mkoani Pwani.

Na Mwandishi Wetu, Kibaha

Rais wa New Covenant Unity International (NCUI) ambaye pia ni Kiongozi wa Huduma ya Sauti ya Uponyaji Tanzania, Nabii Dkt.Joshua Aram Mwantyala amesema kuwa, iwe mvua, iwe jua ataendelea kusimama imara katika maombi kwa ajili ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan,Watanzania na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo muda mfupi mjini Kibaha mkoani Pwani baada ya kutunukiwa cheti cha udaktari wa heshima na Profesa Benezer David wa huduma ya All Nations Christian Church International kutoka Amarilo nchini Marekani.

Nabii Dkt.Joshua amesema kuwa, heshima aliyopewa imetokana na kazi kubwa ambayo amekuwa akiifanya kwa ajili ya Taifa la Tanzania hususani kuongoza Kampeni ya Kuombea Taifa (Pray for Nation) ambayo imewafikia mamilioni ya Watanzania katika mikoa mbalimbali nchini.

“Hii ni heshima ya kipekee, awali ya yote nimshukuru Mungu kwa kuendelea kuniheshimisha ndani na nje ya Tanzania, hatua hii imenipa nguvu na kunitia moyo wa kuhakikisha kuwa ninatumia Biblia Takatifu kueneza habari njema kwa ajili ya kuwaleta pamoja Watanzania na kuhamasisha kila mmoja kufanya kazi kwa bidii ili tuweze kulijenga Taifa letu.

“Katika miaka yangu ya huduma hapa Tanzania, nimefungua makanisa zaidi ya 100 vijijini na mijini,kila mwaka huwa natoa misaada kwa watu maskini,yatima,wajane,walemavu na wagonjwa.
Nimekuwa naandaa makongamano mikoa mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha umoja na kudumisha amani ya nchi yetu ikiwa ni pamoja na kuongoza maombi ya kuombea Taifa na Dunia kwa ujumla.

“Maombi hayo yamekuwa ya baraka mno kwa mamilioni ya watu na shuhuda zimekuwa nyingi sana,hivyo niendelee kusisitiza kuwa, sitarudi nyuma katika kuhubiri neno la Mungu na kuwaleta watu pamoja ili waweze kulijua vema kusudi la Mungu katika maisha yao, hatua ambayo itawawezesha kuishi kwa umoja na mshikamano,”amesema Nabii Dkt.Joshua.

Pia Nabii Dkt.Joshua amesema kuwa, ataendelea kuwa mstari wa mbele katika kusaidia juhudi mbalimbali za maendeleo vijijini na mijini chini ya Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Nimekuwa mdau wa maendeleo na nitaendelea kufanya hivyo kwa kutoa misaada ya umeme jua kwenye vituo vya afya vijijini,kujenga na kukarabati madarasa ya baadhi ya shule za misingi kama niivyofanya awali,”amesema.

Nabii Dkt.Joshua pia amekuwa mstari wa mbele katika kujenga nyumba za familia za polisi na vyoo vya mahabusu pamoja na kuchangia shunguli mbalimbali za maendeleo kwa jamii zenye mahitaji maalumu nchini.

Wakati huo huo, Nabii Dkt.Joshua amesema kuwa, anaendelea na maombi mfululizo kwa ajili ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ili aweze kutekeleza kikamilifu maono ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati Dkt.John Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uwezo wa kujitegemea kiuchumi.

No comments:

Post a Comment