Monday, April 12, 2021

MAFANIKIO YA RUWASA YAOKOA NDOA ZA WANA KATAVI-RC HOMERA

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera

Na Swaum Katambo-Katavi


Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini RUWASA (Rural Water Supply and Sanitation Agency) ilianzishwa kwa Sheria Na. 5 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira ya Mwaka 2019 na ilianza kufanya kazi rasmi mwezi Julai, 2019 na Tangu kuanzishwa kwake Nchini imepata mafanikio makubwa hususani katika Mkoa wa Katavi.


Kabla ya RUWASA kuanza kazi yake Mkoa wa Katavi ulikuwa ukipata maji kwa 42% lakini mpaka sasa imefanikiwa kuongeza 28% na kufikia kuwa na 70% za upatikanaji wa Maji safi na Salama hivyo kupelekea kuhudumia zaidi ya wakazi 500,000 wa Mkoa wa Katavi kwa kipindi cha mwaka mmoja.


Katika mahojiano maalumu na Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera amebainisha baadhi ya Miradi ambayo imetekelezwa kwa kiwango kikubwa ambayo ni Mradi wa Ikolongo II unaotekelezwa kwa zaidi ya Bilioni 3 ambao unasambaza maji katika Wilaya ya Mpanda ukisaidiana na Miradi ya inayoendelea katika Halmashauri ya Nsimbo ikiwemo Manga-Kasokola wenye bajeti ya zaidi ya Milioni 594 ukihudumia zaidi ya wakazi 20,000 huku mradi huo ukiwa umekamilika kwa asilimia 100%.


Mradi wa Maji Mtisi unaohudumia zaidi ya wakazi 3000 umekamilika kwa asilimia 98% ambapo RC Homera ameelezea mafanikio kwa kupunguza changamoto za wananchi kufuata maji Mtoni ambako huko ajali nyingi zilitokea kutokana na jiografia ya mabonde mengi hivyo kwa upande wa kinamama walichelewa kurejea nyumbani na kusababisha ndoa zao kutetereka.


"Hayo ni mafanikio makubwa hivyo RUWASA pia inaboresha ndoa za Watanzania, walio wengi wa Mkoa wetu wa Katavi", Alinukuliwa RC Katavi Juma Homera.


Kadhalika, RUWASA imetekeleza Mradi wa Maji Itenka A na Jilabela Halmashauri ya Nsimbo wa Shilingi Mil 434 unaohudumia zadi ya wakazi 30,000 huku Mradi wa Maji Igongwe-Stalike uliogharimu shilingi Mil 186 ukikamilika kwa asilimia 100% na wakazi zaidi ya 8000 wanaendelea kunufaika na maji hayo ambapo awali wakazi wake walichota maji kwenye Mto wenye wanyama wakali wakiwemo Viboko wengi hali iliyokuwa ikihatarisha maisha yao.


Mradi wa Maji Kanoge line uliopo katika kijiji cha Kanoge Halmashauri ya Nsimbo ni Mradi wa Shilingi Mil 229 wenye Lita za ujazo 100,000 unahudumia zaidi ya wakazi 20,000 ambao umeshakamilika kwa asilimia 98% huku ukipelekea mafanikio makubwa ya wananchi kunufaika na maji safi na salama.


Kwa mafanikio hayo ya  RUWASA katika Mkoa wa Katavi Miradi mingine iliyopo ni Miradi ya Maji Mtapenda, Songambele, na Katika Wilaya ya Tanganyika kuna Miradi ya Maji Mwese, Kamjela, Majalila na Mradi wa Karema uliotumia zaidi ya shilingi Mil 283 ambao umeshakamilika kwa 100%  huku wakazi zaidi ya 14,500 wakinufaika nao.


Kwa mujibu wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) inaelekeza hadi kufikia 2025 upatikanaji wa Maji safi na salama Vijijini uwe zaidi ya asilimia 85% na Mijini asilimia 90% huku Mkoa wa Katavi ukiwa umefanya upembuzi yakinifu kwa maeneo yaliyobaki ya Kata za Katuma, Sibwesa, Mnyagala, Kasekese, Nkungwi, Kaseganyama, Kayenze, Ifumbula, Ikondamoyo na Ibindi ili kujenga miradi mipya ya Maji.


Miradi mingine ni miradi ya Majimoto kutoka kwenye milima ya Lyamba Lyamfipa ambayo zaidi ya wakazi 40,000 wananufaika na maji hayo huku Mkoa ukijipanga kupanua Mradi huo kupeleka maji Ikulwe, Ikuba, Chamalendi na Usevya utakaokwenda kusaidia zaidi ya wakazi 100,000 wa Bonde la Mpimbwe.


Mkuu wa Mkoa wa Katavi Juma Homera anaamini kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao wananchi wa katavi watakata kiu kubwa ya uhaba wa maji kutokana na uwepo wa RUWASA kwa kuwa, kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021 Mkoa huo umepokea zaidi ya Shilingi Bil 7.9 kutoka Serikali kuu ili kutekeleza miradi ya maji iliyopo na itakayoanzishwa lengo likiwa ni kukidhi matakwa ya wananchi wake.


Lengo la Serikali kuanzisha sekta hii ya Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini RUWASA ni pamoja na kuipa majukumu ya Kusanifu na kusimamia ujenzi wa miradi ya maji vijijini, Kufanya utafiti kuhusu maji chini ya ardhi, Kuchimba visima na kujenga mabwawa, Kusajili na kuviwezesha vyombo vya watumiaji maji vijijini, Kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya sekta ya maji vijijini na Kumshauri Waziri wa Maji kuhusu uendeshaji wa sekta ya maji.


MWISHO

No comments:

Post a Comment