MKURUGENZI Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru amesema taasisi hiyo itaendelea kuzingatia miongozo, sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma katika utoaji huduma wa zake kwa wateja.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo watumishi wa HESLB jana (Jumapili Januari, 31 2021), Badru alisema HESLB ni miongoni mwa taasisi za umma zinazogusa maslahi ya makundi mbalimbali ya kijamii, hivyo inawajibika kuweka mikakati madhubuti ya kuhudumia wateja.
Badru alisema kwa kutambua umuhimu huo, Ofisi yake imeandaa miongozo mbalimbali kwa watumishi wake ili kuwajengea uwezo wa namna bora ya kuwahudumia wateja na kushughulikia malalamiko yanayojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
“Mafunzo haya ni sehemu muhimu ya kutukumbusha wajibu wetu katika kuhuhudumia wateja, tukiwa kama taasisi ya serikali tumeendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja kwa kuzingatia miongozo ya utumishi wa umma ikiwemo kuandaa mkataba wa huduma kwa wateja na mwongozo wa kushughulikia malalamiko kwa wateja,” alisema Badru.
Aidha Badru alisema kupitia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika mafunzo hayo, ni wakati muafaka kwa kila mtumishi wa HESLB kutafakari nafasi na wajibu alionao katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa miongozo ikiwemo umuhimu wa kuzingatia uadilifu sehemu za kazi.
“Tunamaliza mwezi Januari tukiwa katika mafunzo haya muhimu yanayotukumbusha utekelezaji wa majukumu yetu, tunapaswa kutimiza wajibu wetu kwa kuzingatia wajibu wa msingi wa kila mtumishi wa umma na kubwa zaidi ni uadilifu katika maeneo yetu ya kazi”, alisema Badru.
Awali, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa HESLB, Neema Kuwite alisema kutokana na umuhimu wa mafunzo hayo, Ofisi yake inaandaa mpango wa mafunzo kwa watumishi kuhusu utekelezaji wa miongozo ya kuhudumia wateja mahali pa kazi kwa kupitia nyaraka mbalimbali ikiwemo mkataba wa huduma kwa mteja ulioanza kutekelezwa na HESLB.
“Kupitia mafunzo haya tumepokea ushauri, maoni na mapendekezo kutoka kwa watumishi kuhusu namna ya kuhudumia wateja wetu, tunaandaa mpango wa mafunzo kwa watumishi ili kuweza kuwajengea uwezo wa pamoja katika kuhudumia wateja wetu”, alisema Kuwite.
Mafunzo hayo ya siku mbili yalishirikikisha jumla ya watumishi 140 kutoka Ofisi ya Makao Makuu ya HESLB, Ofisi za Kanda ya Dodoma, Zanzibar, Mwanza, Mtwara, Arusha na Mbeya.
No comments:
Post a Comment