Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezindua Kampeni Maalum ya kuhamasisha ulipaji kodi ya Pango la Ardhi yenye kauli mbiu inayosema MWAMBIE MMILIKI WA ARDHI, KODI YA PANGO LA ARDHI INAMHUSU.
Katika kampeni hiyo, Maafisa Ardhi na Wajumbe wa Serikali ya Mtaa watasambaza hati za madai ya kodi ya pango la ardhi nyumba kwa nyumba, na Ankara za umilikishwaji maeneo yaliyofanyiwa urasimishaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam tarehe 8 Februari 2021, Naibu Waziri Dkt Mabula aliwakumbusha wamiliki wote wa ardhi nchini kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka usumbufu wa kukamatiwa mali ama kunadiwa mali ili kufidia kodi pamoja na kufutiwa umiliki.
"Kulipa kodi ni kuonesha uzalendo kwa nchi yako na pia ni kuchochea maendeleo ya Taifa, hivyo kodi ya pango la ardhi kama zilivyo kodi nyingine ni muhimu na inachangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kiwango kikubwa" alisema Naibu Waziri Mabula.
Hata hivyo, Dkt Mabula alisema, baadhi ya wamiliki wa viwanja na mashamba hawajatimiza wajibu wao kama yalivyo matakwa ya Sheria, licha ya jitihada zinazofanywa na wataalamu wa Sekta ya ardhi ya kuwakumbusha kupitia mikakati mbalimbali inayotekelezwa sasa.
Aliongeza kwa kusema kwamba, kwa kuwa muda wa kulipa kodi kwa hiyari kisheria umepita na Wizara kupitia watendaji wake imetimiza wajibu wa kuwakumbusha kupitia vyombo vya habari na kuwapelekea hati za madai za siku 14 za kuwataka kulipa bado baadhi ya wamiliki hawajatekeleza.
Ameelekeza Maafisa Ardhi Wateule kote nchini kuanza kuchukua hatua za kisheria chini ya kifungu cha 50 cha Sheria ya Ardhi Na. 4 ya Mwaka 1999 kwa kuwafikisha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya wamiliki wote wa viwanja na mashamba ambao hadi sasa bado hawajalipa kodi ya pango la ardhi kwa kila kipande cha ardhi wanachomiliki.
Vile vile, alisema kwa wamiliki ambao wamevunja masharti ya umiliki kwa kutokulipa kodi na wamepewa hati ya madai chini ya kifungu cha 33(8) na muda wa miezi 6 imepita tangu tarehe ya ilani hizo bila ya kulipa, miliki hizo zibatilishwe kwa mjibu wa Kifungu cha 48(1)(g) cha Sheria ya Ardhi.
Kuhusu misamaha ya kodi ya pango la ardhi kwa Taasisi/Mashirika na Makampuni yasiyotumia ardhi kibiashara, Naibu Waziri wa Ardhi alisema, marekebisho ya Sheria ya ardhi (Sura 113) yaliyofanyika kuhusu msamaha wa kodi ya pango la ardhi na kutangazwa katika Tangazo la Serikali (GN) Na.347 ya tarehe 26/04/2019 yanaelekeza kuwa, msamaha utakaotolewa utazihusu Taasisi/ Mashirika na Kampuni ambazo hazitumii ardhi kibiashara.
Marekebisho hayo yametaja tarehe ya msamaha kuanza 01 Julai 2018, hivyo madeni ya kodi pamoja na malimbikizo yote yaliyokuwepo kabla ya tarehe 01 Julai, 2018 hayafutwi hivyo taasisi hizo zinawajibika kulipa na kusisitiza kwamba, pamoja na sharti la kulipa malimbikizo ya nyuma, maeneo ya biashara yaliyo ndani ya ardhi ya Taasisi au Shirika yataendelea kutozwa kodi ya pango la ardhi.
Alitoa rai kwa Taasisi zenye sifa ya kupata msamaha kuchangamkia fursa hii ikiwa ni pamoja na kufuata masharti yaliyowekwa ikiwemo sharti la kulipa malimbikizo yote kabla ya kuwasilisha maombi ya msamaha.
Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula alisema kuwa, wakati kampeni hiyo ikizinduliwa nchini, mkoa wa Dar es Salaam umekusanya shilingi bilioni 23 kati ya bilioni 62.7 inazotakiwa kukusanya katika mwaka wa fedha 2020/2021.
No comments:
Post a Comment